NEWS

Sunday 28 April 2024

DC Tarime azuru vijiji vilivyoathiriwa na mafuriko bonde la mto Mara, atoa maelekezoMkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Hassan Surumbu (mwenye suruali ya kijivu) akizungumza na wananchi katika kijiji cha Matongo kilichopo bonde la mto Mara, ambako baadhi ya mashamba ya mahindi yameathiriwa na mafuriko.
-----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu/
Mara Online News
---------------------------

MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Hassan Surumbu amefanya ziara ya ghafla katika vijiji vya Matongo na Mrito, na kujionea athari zilizosababishwa na mafuriko ya mto Mara.

Vijiji hivyo vipo ndani ya bonde la mto Mara katika kata za Matongo na Kemambo zilizopo tarafa ya Ingwe wilayani Tarime.

Akiwa kijijini Matongo jana, DC Surumbu alishuhudia mashamba kadhaa ya mahindi yaliyoathiriwa na mafuriko kando kando ya mto Mara.

Aliutaka uongozi wa kijiji hicho kuelimisha wananchi kutojihusisha na shughuli zozote kando kando ya mto huo kipindi hiki cha mvua nyingi, ili kuepuka hatari za kusombwa na maji, na kuuawa na wanyama kama vile mamba na kiboko.

Hata hivyo, kiongozi huyo aliipongeza Serikali ya Kijiji cha Matongo kwa kusimamia sheria na kuhakikisha wananchi hawajengi makazi kando kando ya mto huo.Kuhusu mashamba yaliyoathiriwa na mafuriko, DC Surumbu aliwaagiza wataalamu wa kilimo kufanya thathmini ili serikali iweze kutafuta wadau wa maendeleo watakaosaidia upatikanaji wa mbegu za mazao ya chakula ili kuwezesha wakulima husika kupanda msimu ujao.

Kuhusu mamba na kiboko wanaotishia maisha ya watu katika vijiji vya Mrito na Matongo, mkuu huyo wa wilaya aliahidi kufikisha suala hilo kwa maafisa wa wanyamapori kwa hatua za ufumbuzi.

Hata hivyo, aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanachukua tahadhari muda wote ikiwa ni pamoja na kutojaribu kuvuka “maji yanayotembea”.


DC Surumbu (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa wananchi kando ya mto Mara katika kijiji cha Mrito.
------------------------------------------------

Katika hatua nyinyine, DC Surumbu alitembelea familia ya Mwita Marembera Mwita iliyokumbwa na mkasa wa kubomokewa ukuta wa nyumba katika kitongoji cha Sukube kijijini Kewanja, na kuelekeza wataalamu husika kufanya tathmini ya madhara yaliyotokea ili ofisi yake iangalie namna ya kusaidia.

Katika ziara hiyo, DC Surumbu alifuatana na Afisa Tarafa ya Ingwe, James Yunge, miongoni mwa viongozi wengine.

Siku chache kabla ya DC Surumbu kufanya ziara hiyo, Mara Online News iliripoti kuwepo kwa madhara ya mafuriko katika bonde la mto Mara, ambapo inadaiwa kuwa wananchi zaidi ya 1,500 wako hatarini kukumbwa na baa la njaa kufuatia mashamba yao ya mahindi kujaa maji.

Baadhi ya wananchi walisema hawana mategemeo ya kuvuna chochote baada ya mashamba yao kujaa maji.“Tunategemea haya mahindi lakini sasa mashamba yamejaa maji, tuna watoto, hatujui watakula nini, tunaomba msaada,” alisema mkazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Maningo.

“Haya ni mafuriko na msimu uliopita pia hatukuvuna, cha kwanza tunaomba msaada wa chakula, cha pili tunaomba mbegu,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matango, Daudi Itembe aliwambia waandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages