NEWS

Saturday 27 April 2024

Rorya: Ubovu wa barabara wawatesa wananchi kijiji cha Irienyi




Na Mwandishi Wetu/
Mara Online News
---------------------------


WANANCHI wa kijiji cha Irienyi katika wilaya ya Rorya mkoani Mara, wanakabiliwa na kero ya muda mrefu ya ubovu wa barabara muhimu wanayotumia katika safari za kujitafutia riziki na mahitaji ya kifamilia.

“Kuharibika kwa barabara hii ni kero kubwa kwa wananchi wa Irienyi na vijiji jirani, inakwamisha na kuchelewesha safari za wananchi, maana imegeuka kuwa mtaro wa maji,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Irienyi, Steven Mwikwabe ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo asubuhi.

Mwikwabe amebainisha kuwa barabara hiyo inaanzia njia panda ya kwenda Misheni na mnada wa Nyamaguku hadi kwenye skimu ya umwagiliaji ya Irienyi.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, barabara hiyo ina urefu wa kilomita saba lakini sehemu iliyoharibika zaidi ni kilomita mbili. “Wananchi wanatembea kwenye maji, na vyombo vya usafiri vinapita kwa shida sana,” amesema.

“Barabara hii iko chini ya TARURA (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini). Mwaka jana Mbunge [wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege] alisema ilikuwa imetengewa bajeti ya kutengenezwa lakini mpaka sasa hivi hatujaona chochote,” amesema Mwikwabe.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kupata majibu ya mamlaka husika kuhusu kero hiyo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages