NEWS

Monday 27 May 2024

AICT, Right to Play watajwa kupunguza ukatili wa kijinsia katika jamiiMwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marenga B iliyopo wilayani Serengeti, Rahabu Ketocho akikabidhi kombe kwa mwakilishi wa washindi.
-------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Serengeti
----------------------------------------


Jamii imeeleza kuridhishwa na uhamasishaji wa haki sawa kwa watoto wa kike - ikiwemo ya kupata elimu bora, unaotolewa na Shirika la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe.

Kwamba uhamasishaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ukatili kwa watoto wa kike na kuchochea mahudhurio yao shuleni.

Hayo yalisemwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marenga B iliyopo wilayani Serengeti, Rahabu Ketocho wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililoandaliwa na AICT na Right to Play.Tamasha hilo lilifanyika juzi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Merenga A kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

"Wamepunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia, mfano baada ya kutoa elimu ukeketaji umepungua, vipigo kwa watoto wa kike vimepungua, uandikishaji wao shuleni umeongezeka na hata uwezo wao wa kitaaluma umeongezeka, ambapo katika mitihani yetu ya mara kwa mara wanafaulu vizuri,” Mwalimu Rahabu.

Aidha, alilishukuru Shirika la Right to Play kwa kufadhili ujenzi wa chumba cha darasa katika Shule ya Msingi Merenga B, kupeleka vifaa mbalimbali vya kufundishia na kuwajengea walimu na wanafunzi uwezo kupitia michezo."Ukipita Shule ya Msingi Merenga B kwa uwazi kabisa utaona darasa zuri liko pale limejengwa kwa shilingi zaidi ya milioni 34, ni la kisasa kabisa, na hizo ni nguvu za Right to Play, lakini pia ukifika hapa Merenga A utaona wametuletea zana za kujifunzia, kufundishia na walimu wamepata mafunzo kupitia michezo," alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Charles Mashauri alisema taasisi hizo zinashirikiana kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutoa haki sawa kwa watoto wa kike ikiwemo ya kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wa kiume.


Tamasha hilo la michezo kwa wanafunzi lilifanyika chini ya mradi wa AICT na Right to Play unaojulikana kama "Save her seat" ikimaanisha "Linda kiti cha mtoto wa kike".

Lilihudhuriwa pia na wafadhili wa mradi huo kutoka nchini Uingereza na Mkurugenzi Mkuu wa Right to Play Tanzania, Maria Mongi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages