NEWS

Monday 6 May 2024

RPC athibitisha kifo cha raia na askari polisi kujeruhiwa Nyamongo, aonya wavamizi wa mgodi



Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Polisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Mei 6, 2024.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
----------------------------


Jeshi la Polisi limethibitisha kifo cha raia mmoja na kujeruhiwa kwa askari polisi mmoja pia katika kijiji cha Kewanja - Nyamongo wilayani Tarime katika mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Polisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera, tukio hilo lilitokea jana saa 12 jioni kijijini hapo wakati watu waliokuwa na silaha za jadi waliposhambuliana na askari polisi waliokuwa wakiwazuia kuvamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Akitoa taarifa hizo kwa waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda Njera amemtaja raia aliyepoteza maisha kutokana na mashambuliano hayo kuwa ni Emmanuel Nyakoringa (36), na kwamba askari (hakumtaja) aliyejeruhiwa na anaendelea na matibabu.

“Mashambulizi ya watu hao kwa askari yalidumu kwa takribani nusu saa,” amesema RPC huyo.

Hata hivyo, amesema askari walifanikiwa kuwadhibiti na kuwatawanya watu hao.

“Uchunguzi wa tukio hili unaendelea ili kuweza kuchukua hatua za kisheria zinazostahili kwa wahusika,” ameongeza.

RPC Njera ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya uhalifu vikiwemo vya kuvamia mgodi kwani Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria.

“Tunawataka wananchi kutii sheria bila shuruti kwani hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote anayekiuka sheria za nchi,” amesisitiza Kamanda Njera

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages