NEWS

Wednesday 22 May 2024

Kiles atoa msaada wa vifaa kukamilisha ujenzi Kituo cha Polisi Borega- Tarime Vijijini



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles (katikati) akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili aliotoa kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Borega jana Jumanne. (Picha na Mara Online News)
-------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
------------------------------------


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Borega katika kata ya Ganyange.

Sambamba na vifaa hivyo, Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga kwa tiketi ya chama tawala - CCM, amekabidhi shilingi laki nne kwa ajili ya malipo ya fundi wa ujenzi huo.

"Hiki kituo ni cha kwetu wote kwa ajili ya ulinzi wa jamii, tutaendelea kusaidiana na kushirikiana, hapa ni mpakani na nchi jirani, wizi wa mifugo umepungua, tuko kwa ajili ya kuhudumia wananchi," alisema Kiles wakati wa hafla ya makabidhiano hayo kituoni hapo jana Jumanne.

Mkuu wa Kituo hicho, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Maulidi Rashidi Ahungu alimshukuru Mwenyekiti Kiles kwa msaada huo na kuomba ushirikiano wa wananchi katika kuimarisha usalama kwenye eneo hilo.

"Tunakushukuru Mwenyekiti wa Halmashauri kutushika mkono kwa kutuletea vifaa hivi ukizingatia kituo hiki kipo mpakani, wananchi na mali zao zitakuwa salama, tunaomba waendelee kuwa na imani na Jeshi la Polisi kwa kutoa ushirikiano ili kuendelea kudumisha amani na usalama," alisema Inspekta Ahungu.

Nao wananchi wa eneo hilo walimshukuru Mwenyekiti Kiles kwa kuguswa na adha ya matukio ya uhalifu yaliyokuepo siku za nyuma ukiwemo wizi wa mifugo, na hivyo kuona umuhimu wa kujitolea kuchangia ukamilishaji wa kituo hicho kilichojengwa kwa nguvu zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages