NEWS

Tuesday 21 May 2024

CHADEMA kuchochea mchuano mkali CCM Tarime Vijijini 2025




Na Ambrose Wantaigwa, Tarime
-------------------------------------------


Kuna kila dalili za kutokea mchuano mkali wa kuwania kuteuliwa kugombea kiti cha ubunge mwaka 2025 katika jimbo la Tarime Vijijini kupitia CCM, huku baadhi ya makada maarufu wa chama hicho tawala wakihusishwa na mbio hizo.

Hii ni kutokana na jimbo hilo kuwahi kuwa ngome ya chama cha upinzani - CHADEMA kwa vipindi vitatu.

Kwa mujibu wa mjumbe wa zamani wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilayani ya Tarime, Laurent Nyablangeti, chama hicho kinapaswa kuteua wagombea wanaoweza kukidhi matakwa ya wapigakura ili kushinda siasa za upinzani.

"Wakati huu tukielekea kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, lazima CCM tuhakikishe tunajiandaa kuweka wagombea wanaoweza kutatua kero za wananchi kwa haraka, ukizingatia eneo hili lina upinzani wa kiasi," Nyablangeti aliiambia Mara Online News mjini Sirari juzi.

Alifafanua kuwa kwa muda mrefu wapinzani jimboni humo waliwekeza katika matatizo sugu ya wananchi yaliyokosa utatuzi, ikiwemo migogoro ya sekta ya madini sanjari na wakazi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

"Hata hivyo kuna ahadi zilizotolewa na serikali katika uchaguzi mkuu uliopita, ikiwemo ugawaji wa mamlaka za utawala na kupandisha hadhi maeneo ya vijiji kuwa mamlaka ya miji midogo kama Sirari na Nyamongo bado zinashughulikiwabado," aliongeza.

CCM wanajipanga kupata wagombea wa serikali za mitaa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani katika jimbo hilo ambalo lilikuwa chini ya John Heche kupitia CHADEMA mwaka 2015-2020, ambaye alishatangaza kugombea tena kiti hicho.

Miongoni mwa makada wanaotajwa kuleta msisimko ndani ya uteuzi wa CCM jimboni humo, ni pamoja na mbunge wa sasa Mwita Waitara ambaye tayari alishatangaza kutetea kiti chake katika vikao mbalimbali nje na ndani ya jimbo.

Wengine ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi ambaye ingawa bado hajatangaza rasmi anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wenye nguvu za kuweza kuomba kuteuliwa na chama hicho.

Maswi ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, anawakilisha kundi la wasomi na watumishi wa serikali ambao wanatajwa kusababisha mchuano mkali ndani ya CCM wakati ukifika, kutokana na historia ya jimbo hilo la mpakani na nchi jirani ya Kenya.

Katika orodha hiyo yumo pia aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Tarime kupitia CCM, Nyambari Nyangwine ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd (NNGCL).

Nyambari alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, akimbwaga Mwita Waitara aliyegombea kwa tiketi ya CHADEMA.

Nyambari aliongozi jimbo la Tarime hadi mwaka 2015, ambapo Christopher Kangoye aliteuliwa na CCM kugombea ubunge wa jimbo hilo, lakini alishindwa na John Heche wa CHADEMA.

Awali, jimbo hilo lilipata umaarufu mwaka 2005 baada ya CHADEMA kupata ushindi wa kwanza katika siasa za vyama vingi kupitia mbunge machachari Chacha Zakayo Wangwe ambaye hata hivyo alifariki dunia kwa ajali ya gari mwaka 2008.

Uchaguzi mdogo ambao ulihusishwa na vurugu zilizosababisha uharibifu wa mali na vifo, ulifanyika na chama hicho cha upinzani kilishinda kupitia Charles Mwera ambaye alihudumu mpaka 2010 ambapo CCM ilishinda tena kupitia kwa Nyambari Nyangwine.

"Kawaida kanuni zetu haziruhusu kufanya kampeni wakati kuna mbunge hajamaliza muda wake, lakini kila mwanachama ana uhuru wa kutoa maoni yake bila kuathiri umoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama [CCM] wakati wote," alisema Nyablangeti.

Katibu wa mbunge wa jimbo hilo, Remmy Mkapa alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM unaendelea, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari na barabara pamoja na kusimamia ulipwaji fidia kwa wakazi wanaopisha uwekezaji katika mgodi wa North Mara.

"Hivi sasa bado tu upandishwaji wa mji wa Sirari na Nyamongo kuwa mamlaka ya mji mdogo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ili kuongeza nguvu ya ushindi wa Chama Cha Mapinduzi muda wote," alisema Mkapa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages