NEWS

Wednesday 15 May 2024

Mkuu wa Mkoa awaagiza Ma-DC, Ma-DED kusaidia utatuzi wa migogoro ya ardhi inayovikabili vyama vya ushirika MaraSehemu ya washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara ulioanza leo Jumatano mjini Musoma.
--------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Musoma
--------------------------------------


Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuingilia kati utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyopo kati ya vyama vya ushirika, taasisi za umma na watu binafsi mkoani humo.

“Migogoro hii imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya sekta ya ushirika… nawaelekeza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kukaa na wanaushirika na kupitia changamoto hii, kisha kwa pamoja kutafuta nama ya kuikabili,” amesema.

RC Mtambi ametoa maelekezo hayo wakati akihutubia mkutano wa siku mbili wa Jukwaa la Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mara, ulioanza leo Jumatano katika ukumbi wa CCM mjini Musoma.

Aidha, amevikumbusha vyama vikuu vya ushirika, yaani WAMACU Ltd na PMCU kusimamia vizuri vyama vya msingi na kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wenye tija katika mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa na pamba.

Pia RC Mtanda amevitaka vyama hivyo kuhakikisha kuwa madeni viliyokabidhiwa na iliyokuwa MCU Ltd yanalipwa kwa wakati. “Kwa kufanya hivyo kutajenga na kuimarisha taswira ya ushirika wa kibiashara kwa manufaa ya kiuchumi kwa jamii yetu,” amesema.

Sambamba na hilo, amewakumbusha viongozi wa vyama hivyo kusimamia kikamilifu mali za ushirika, kufanya vikao na kusoma taarifa kwa wanachama kwa uwazi.


RC Mtambi akizungumza 
katika mkutano huo.
-------------------------------------------------------

Kuhusu msimu wa ununuzi wa pamba uliozinduliwa kitaifa Mei 8, mwaka huu, RC Mtambi amewaelekeza viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) kusimamia vizuri shughuli hizo na kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao.

“Maafisa ushirika wafuatilie kwa karibu ununuzi wa pamba na kutoa taarifa kwa wakuu wa wilaya endapo wataona kuna mwenendo usiofaa, ikiwa ni pamoja na changamoto ya wakala wa upimaji,” ameagiza.

Kiongozi huyo wa mkoa ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wanaushirika kila mmoja kwa nafasi yake kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages