NEWS

Monday 27 May 2024

RUWASA Mara yaingia Nyanungu kwa kishindo, mamia ya wananchi kupata maji ya bomba, Diwani atia neno



Sehemu ya mabomba yaliyopelekwa na RUWASA katani Nyanungu kwa ajili ya ujenzi wa maji ya bomba.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
----------------------------


Ni tabasamu tupu. Ndivyo tunavyoweza kuelezea furaha iliyowajaa wananchi wa kata ya Nyanungu kutokana na kufikiwa na mradi wa maji ya bomba kwa mara ya kwanza (wenyewe wanasema tangu dunia iumbwe).

Kata ya Nyanungu inaundwa na vijiji vinne kaskazini-mashariki mwa wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Kwa upande wa mashariki inapakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti iliyo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Wananchi wa kata hiyo wamefunguka ya moyoni baada ya kuona Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA) imejitokeza kuwajengea mradi mkubwa wa maji ya bomba.

Wanasema mradi huo utawakomboa kwa mambo mengi, ikiwemo kuwapunguzia migogoro na Hifadhi ya Taifa Serengeti kutokana na utafutaji wa maji ya matumizi ya nyumbani na mifugo yao.

“Tulidhani ni ndoto, tunaishukuru RUWASA na Serikali ya CCM chini ya Mama Samia [Rais Dkt Samia Suluhu Hassan], mradi huu utapunguza vurugu kati ya wananchi wa vijiji vya kata hii na TANAPA kwa kuwa vyanzo vingi vya maji viko hifadhini,” anasema Mohere Chacha Moragiri, mkazi wa kijiji cha Kegonga.


Mohere Chacha Moragiri
--------------------------------------

Moragiri ni miongoni mwa wananchi kadhaa waliozungumza na Sauti ya Mara kuhusu mradi huo katani Nyanungu wiki iliyopita.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Matinde Marwa anasema: “Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha usalama kwa akina mama kwa kuwawezesha kupata maji karibu, maana visima vingi hapa Kegonga vipo mbali - mpakani mwa nchi jirani ya Kenya, na vingine vipo ndani ya Hifadhi ya Serengeti ambapo kuna wanyama hatari - tunapokwenda kutafuta maji nyakati za usiku.”

Mjasiriamali maarufu kwa biashara ya mama lishe kijijini Mangucha, Nyamugi Petro anasema ujio wa mradi huo ni mageuzi makubwa katika sekta ya maji katani Nyanungu.

“Tunaupokea mradi huu kwa mikono miwili, hii ni historia tangu tupate uhuru, ni haki yetu tuanze kupata ladha ya maji ya serikali hapa Nyanungu. Huu ni wakati wa sayansi na teknolojia, wenye vyoo vya kisasa maji haya yatarahisisha huduma, hususan siku za soko,” anasema Nyamugi.


Nyamugi Petro
-----------------------

Nyamohanga Meck naye ni mkazi wa Mangucha, anasema: “Hii ni fursa kwetu vijana, tutaanzisha miradi ya ‘car wash’ pamoja na bustani za miche ya miti mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha kipato. Lakini pia mradi huu utatuepushia milipuko ya magojwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama, kwani tuna soko linalokaa kila wiki.”

Faida nyingine za mradi huo zinatarajiwa kuonekana kwenye shule za msingi na sekondari katani Nyanungu.

“Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha huduma ya maji katika shule za msingi na sekondari katani kwetu, na hivyo kuchangia kuinua taaluma kwa wanafunzi, ukizingatia sekondari ya Nyanungu imeidhinishwa kuwa ‘high school’.

“Hakika hili ni jambo la kujivunia, Mama Samia ameamua kutujali kwa kumtua mama ndoo ya maji kichwani,” anasema Neema Sandwe, mkazi wa kijiji cha Nyamombara.

"RUWASA wamefanya jambo muhimu katika maisha yetu, tumechoka kuchangia maji na wanyamapori, tunaishukuru Serikali ya Mama [Rais Samia] kutukumbuka," anasema Nyambari Nchagwa, mkazi wa kijiji cha Nyandage.


Nyambari Nchagwa
----------------------------

Naye Diwani wa Kata ya Nyanungu kwa tiketi ya chama tawala - CCM, Tiboche Richard anaishukuru RUWASA na serikali kwa ujumla kwa kuwakumbuka wananchi wa kata hiyo kwa mradi huo wa maji ya bomba.

“Tumeupokea mradi huu kwa furaha kubwa, ni mradi mkubwa - una thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja. Ukikamilika utahudumia vijiji vine. Toka dunia iumbwe hatujawahi kupata mradi hata wa kisima.

“Rai yetu kwa wananchi, ni kuhifadhi vyanzo vya maji ili mradi huu uwe endelevu. Huu ni mradi wa mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - utakaokuwa kichocheo cha kura nyingi za ushindi kwa chama chetu cha CCM katika uchaguzi ujao wa udiwani, ubunge na Rais,” anasema Tiboche.


Ujenzi wa tenki la maji 
unaendelea kijijini Kegonga
------------------------------------------------

Utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa matenki mawili ya maji na utandazaji wa mabomba kuwezesha wananchi kupata huduma kupitia vituo maalumu na mabomba majumbani.

“Tenki moja lenye ujazo wa lita 100,000 linajengwa katika kijiji cha Kegonga na jingine lenye ujazo wa lita 50,000 linajengwa mpakani mwa kijiji cha Mangucha na Nyamombara,” anafafanua Mhandisi Mohamed Mtopa kutoka RUWASA Wilaya ya Tarime.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mtopa, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika na kuanza kusambaza huduma ya maji kwa wananchi Desemba 2024.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages