NEWS

Wednesday 26 June 2024

AICT, Right to Play hakuna kulala vita mila za kikatili kwa watoto wa kike Tarime



Viongozi wakikabidhi zawadi ya jezi kwa wanafunzi walioshiriki tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Right to Play, kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Gwitare wilayani Tarime leo.
------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime
------------------------------------

Jamii wilayani Tarime, Mara imehamasishwa kuacha mila potofu zinazopelekea vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

Hamasa hiyo imetolewa wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililoandaliwa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play.

Tamasha hilo limefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Gwitare iliyopo kata ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, leo Jumatano.

Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo ametumia fursa ya tamasha hilo kuhamasisha jamii kuzingatia umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, sambamba na kutokomeza ukatili dhidi yao.

"Sisi tunaendelea kuihamasisha jamii hasa katika maeneo haya ya Gwitare kuachana na vitendo vya ukeketaji, ndoa za utotoni na namna zozote zinazomzuia mtoto wa kike kupata elimu, ndiyo maana tunayo klabu yetu hapa ya 'Save Her Seat' inayomfunza mtoto wa kike namna ya kukabiliana na changamoto,” amesema Fungo.

Fungo akizungumza tamashani
----------------------------------------

Kwa upande wake Miriam Samwel ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Gwitare na mwanachama wa klabu hiyo ya 'Save Her Seat', amezishukuru taasisi hizo kwa jitihada zinazoonesha katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto wa kike, pamoja na kuwapatia mafunzo mbalimbali.

"Mimi nawashukuru AICT na Right to Play kwa juhudi zao za kutusaidia dhidi ya ukatili, mfano mimi tangu nimejiunga na klabu ya Save Her Seat nimetambua haki zangu na umuhimu wa elimu, lakini pia nimejifunza vitu vingine vingi vinavyonisaidia kupambana na baadhi ya changamoto,” amesema Miriam.

Naye msimamizi wa mradi wa Save Her Seat katika kituo cha Gwitare, Penina John amesema elimu na zawadi mbalimbali zinazotolewa na AICT na Right to Play kwa wanafunzi, zimesaidia kuchochea mahudhurio ya watoto wa kike shuleni na pia uwezo wao darasani umeongezeka.

AICT na Right to Play wamekuwa wakishirikiana kutoa hamasa kwa jamii za mkoani Mara juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, pamoja na kuachana na mila kandamizi kwao kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo huo wa Save Her Seat (Linda Kiti cha Mtoto wa Kike) unaojikita kuelimisha jamii na kuwafundisha watoto wa kike namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages