Sehemu ya washiriki wa mdahalo wa fursa za uwekezaji ulioandaliwa na Right Way kwa kushirikiana na Mara Online mjini Tarime.
---------------------------------------------------
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------
Makundi mbalimbali ya jamii katika wilaya ya Tarime yameshiriki mdahalo wa aina yake wa fursa za uwekezaji - ulioandaliwa na Right Way kwa kushirikiana na Mara Online News.
Mdahalo huo wenye kaulimbiu inayosema “Fursa za Uwekezaji Zinaanza na Mimi”, umefunguliwa na Mkuu wa Wilaya, Kanali Maulid Surumbu aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, mjini Tarime leo Jumanne.
Katika hotuba yake, Kanali Surumbu amewashukuru waandaaji wa mdahalo huo, akisema umewapa washiriki nafasi ya kujadili namna vijana kama si wananchi wote wilayani Tarime wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo bila kuhatarisha maisha yao na kusababisha taharuki katika jamii.
“Ni muhimu kuwa na majadiliano ya namna hii ili wanajamii wabainishe fursa zilizopo na changamoto zinazowakabili, na kwa pamoja watafute suluhisho kwa manufaa yao,” amesema Kanali Surumbu.
Kanali Surumbu ametoa mfano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), akisema una fursa za ajira na usambazaji wa huduma mbalimbali, ambapo wazawa wa vijiji vinavyouzunguka wanapewa kipaumbele.
“Dhahabu inayozalishwa itafikia kipindi itaisha, lakini maisha ya wana-Tarime lazima yaendelee, ndiyo maansa serikali ikatunga Sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content), ili wakati wa uhai wa mgodi wananchi watumie vyema fursa hizi kujiletea njia mbadala za maendeleo.
“Ninaambiwa pale Nyamongo kuna kampuni [Ress) iliyoanzishwa na mabinti wawili ya kuosha ma-dumper, lakini leo ni kampuni kubwa ya ujenzi, ina vifaa vyake na imeajiri vijana wasomi.
“Vijana hawa ambao walianza wakiwa chini kabisa, mgodi ukifika kikomo bado wanaweza kuendelea kuajiri watu kwa kufanya kazi sehemu nyingine nchini, kwa kuwa tayari wanao mtaji na uzoefu,” amesema Kanali Surumbu.
Kanali Surumbu akifungua mdahalo huo.
----------------------------------------------------
Wachangiaji wengi wa mada katika mdahalo huo wameunga mkono kauli hiyo ya Mkuu wa Wilaya na kutuma wito kwa vijana wanaoishi jirani na mgodi wa North Mara kutumia njia sahihi kunufaika nao, badala ya kuuvamia na kuiba mawe ya dhahabu.
Pia wengi wao wamesisitiza suala la kuendelea kuelimisha vijana na jamii kwa ujumla juu ya umuhimu na faida za mgodi huo na madhara ya kuuvamia.
Awali, Mratibu wa mdahalo huo, Deus Bugaywa amesema wameuandaa kwa lengo la kuhamasisha maelewano na amani kati ya wanajamii na mgodi wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mdahalo huo umehudhuriwa na makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wazee wa mila, viongozi wa dini, madiwani, vijana, Jeshi la Polisi, maafisa maendeleo ya jamii, walimu, wanafunzi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
No comments:
Post a Comment