Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob.
------------------------------------------------
Na Mwandishi wa
Mara Online News
-------------------------
Mara Online News
-------------------------
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko amempongeza Mugini Jacob kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC).
“Nimepokea taarifa ya ushindi huo kwa furaha, klabu zetu zinahitaji watu wenye maono kama Jacob na sasa tunaweza hata kufanya mashirikiano na Mara Regional Press Club,” Soko ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu mapema leo Jumamosi.
Jacob aliibuka mshindi wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliofanyika mjini Musoma jana Ijumaa, ambapo alivuna kura 14 dhidi ya mshindani wake, Anthony Mayunga aliyepata kura 10 na kukubali matokeo hayo.
"Huu sio ushindi wa Mugini, bali ni ushindi wa MRPC," alisema Mayunga ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe katika mkoa wa Mara, na mmiliki wa vyombo vya habari vya Serengeti Media Centre na ANTOMA Online TV.
Aidha, wajumbe wa mkutano huo walimchagua Mohamed Nyabange kuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya MRPC kwa kura 12, akimshinda Ghati Msamba kwa kura moja kwenye kura za marudio baada ya kulingana kipindi cha kwanza ambapo kila mmoja alipata kura 12.
MRPC ni moja ya klabu kongwe nchini ambazo ni wanachama wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Baada ya kutangazwa mshindi, Jacob aliwashukuru wanachama wote wa MRPC kwa kumpatia kile alichokiita ushindi wa kihistoria kwa klabu hiyo.
Jacob akizungumza baada ya kuchaguliwa.
----------------------------------------------------
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kurudi kuwa Mwenyekiti wa MRPC, hii ni mipango ya Mungu, nawashukuru wote mlionipa kura na ambao hamkunipa, sasa sisi ni kitu kimoja na huu ni ushindi wa MRPC,” Jacob ambaye pia ni Mkurugenzi na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara alisema katika sehemu ya hotuba yake ya shukrani kwa waandishi wa habari wa mkoa huo.
Jacob ambaye kitaaluma ni Mwandishi wa Habari mwenye Shahada (Digrii) ya Mawasiliano ya Umma, na Stashahada (Diploma) ya Mahusiano ya Umma (PR), pia amewahi kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya kitaaluma ndani na nje ya nchi, ikiwemo Ujerumani na Uholanzi.
Mugini Jacob (kushoto) na mwanataaluma mwenzake wakiwa wakiwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari jijini Bonn, Ujerumani.
-----------------------------------------------------
Mugini Jacob akiwa kazini.
----------------------------------
Aidha, Jacob amewahi kuripotia vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa kwa zaidi ya miaka 18.
Hivyo baada ya kuchaguliwa jana aliahidi kushirikiana na viongozi wenzake katika kuifanya MRPC kuwa Press Club bora na kimbilio la waandishi wa habari katika mkoa wa Mara wenye waandishi wa habari zaidi ya 50.
Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob (katikati), Makamu wake, Raphael Okello (wa pili kulia), Katibu Mtendaji wa klabu hiyo, Pendo Mwakyembe (wa pili kushoto), wajumbe wa Kamati Tendaji na Anthony Mayunga (mwenye shati la drafti nyuma) ambaye Jacob alishindana naye, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya uchaguzi huo. (Picha na Mara Online News)
-----------------------------------------------------
No comments:
Post a Comment