NEWS

Wednesday 19 June 2024

Vijana wilayani Tarime waalikwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba yanayofanyika katani MwemaKatibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye (mwenye shati jeupe) akishiriki kuhamasisha mafunzo ya Jeshi la Akiba yanayofanyika katani Mwema.
------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Tarime
------------------------------------


Vijana wa kiume na kike katika wilaya ya Tarime mkoani Mara wanakaribishwa kujitokeza kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) yanayofanyika katika kijiji cha Korotambe kilichopo kata ya Mwema.

“Mafunzo haya yalianza wiki mbili zilizopita, na tuna wiki moja ya kuendelea kupokea vijana wengine wenye utayari wa kuja kushiriki mafunzo haya,” Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye amesema wakati wa uzinduzi rasmi wa mafunzo hayo leo Juni 19, 2024.

Kwa mujibu wa DAS Mwaisenye, usajili wa vijana wanaohitaji kujiunga na mafunzo hayo wenye umri wa kuanzia miaka 18 unatarajiwa kufungwa Juni 26, 2024.

“Kwa hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Hassan Surumbu, ninawalika vijana wa kiume na kike waje kujiunga na mafunzo haya kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

“Mafunzo haya yana faida mbili; moja ni kwa Taifa ambayo ni kuongeza walinzi wa amani nchini, lakini pili ni kwa vijana wenyewe binasi kwa sababu kuna ajira nyingi kupitia JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) na Jeshi la Akiba,” amesema Mwaisenye.

Ameelekeza vijana ambao hawafahamu kilipo kijiji cha Korotambe, kufika ofisi ya Mshauri wa Jeshi la Akiba zilizopo mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, ili kupata urahisi wa kujiunga na mafunzo hayo.

DAS Mwaisenye ametumia nafasi hiyo pia kuwapongeza vijana waliokwishafika kujiunga na mafunzo hayo, na kuwataka kuhakikisha wanayakamilisha kwa ufanisi.

“Mkuu wa Wilaya Kanali Maulid Hassan Surumbu atatoa ng’ombe na mimi kama msaidizi wake wa karibu nitatoa mchele kwenye sherehe za kuhitimu mafunzo haya,” amesema DAS Mwaisenye.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages