Na Mara Online News, Tarime
----------------------------------------
----------------------------------------
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara jana alikumbwa na wakati mgumu wa wananchi kumpokea kwa yowe, matusi na mabango ya kumkataa alipokwenda kushiriki mapokezi ya mwili wa kijana Justin Mataro (28) katani Sirari.
Kijana huyo alifariki dunia Juni 15, mwaka huu katika ajali ya gari iliyotokea katani Itiryo na kujeruhi wengine 17 wakati wakitoka kwenye fainali ya mashindano ya Kombe la Waitara yaliyopewa jina la Waitara Cup.
Baadhi ya mabango yaliyooneshwa wakati Waitara alipowasili eneo la msiba huo katani Sirari yalisomeka: “CCM MKILAZIMISHA KURUDISHA WAITARA MTAKIONA CHA MTEMA KUNI”, “KWA KUNUSURU CCM MSIRUDISHE WAITARA TENA”, “HATUMTAKI WAITARA TENA SIRARI” na “MBUNGE WAITARA ACHA KUTUTOWA KAFARA SIRARI.”
Hata hivyo, alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu leo kuhusu mashambulizi hayo dhidi yake, Waitara amedai kuwa yote yaliyomkuta huko Sirari yalitengenezwa na mahasimu wake wa kisiasa, na kwamba aliyajua mapema kabla ya kwenda huko.
“Mimi haikunishitua kwa sababu ni kitu ambacho nilikuwa najua kwamba kimepangwa, nilikuwa na information hizo tangu msiba wa huyo kijana ulipotokea - walianza kusema mimi nimetoa kafara,” amesema Waitara.
Inaelezwa kuwa kijana Justin Mataro aliyefariki dunia na wenzake 17 waliojeruhiwa walikuwa wachezaji na mashabiki wa timu ya Sirari FC iliyotwaa ubingwa wa mashindano ya Waitara Cup na kupata zawadi ya kombe na fedha taslimu.
Mwili wa kijana Justin Mataro unatarajiwa kupumzishwa kwenye nyumba ya milele leo katani Sirari, na mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM amesema atashiriki mazishi hayo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
- 1.HAIPPA PLC inavyoshagihisha uwekezaji Tanzania .
- 2. Musoma Vijijini wanavyopiga hatua ujenzi shule za sekondari za kata .
- 3.Rais Samia atembelea Sekondari ya Seminari ya Kaengesa mkoani Rukwa .
- 4.Waridi wa BBC: Rushwa ya ngono inazima ndoto za wasichana wengi .
- 5.Siasa:Nape aomba radhi kutokana na kauli yake ya ‘ushindi nje ya boksi’ .
No comments:
Post a Comment