NEWS

Wednesday 3 July 2024

Rais Samia asisitiza ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi za Dini, ampongeza Askofu Pisa kwa kuchaguliwa Rais TEC



Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa (kushoto) akifurahia kupokea zawadi ya picha yake kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mkoani Lindi leo.
--------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Waziri Mkuu (PM) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anasisitiza ushirikiano wa kazi kati ya Serikali na Taasisi za Dini nchini, ili kuendelea kujenga amani, umoja na mshikamano.

Amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hizo, ambao huleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa.

PM Majaliwa ameyasema hayo mkoani Lindi leo, wakati akiwasilisha Salamu za Pongezi kutoka kwa Rais Dkt Samia, kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi.

“Tunashukuru tunapata ushauri, yapo mambo ambayo mnayafanya na kuiwezesha nchi hii iendelee, mshikamano wetu ndani ya nchi, umoja wetu ndio unaozaa utulivu na amani tuliyonayo,” amesema.

Amesema kuwa serikali itaendelea kumpa ushirikiano wa dhati. “Wakati wote utakapokuwa na jambo ambalo unadhani serikali inahitaji kushauriwa uwe huru na wakati wote unapoona kwamba unahitaji kuunganisha nguvu na serikali, sisi tutakupa ushirikiano.”

Ameongeza kuwa serikali kwa upande wake imeshaagiza ushirikiano huo, na usiwe tu ngazi ya kitaifa, bali uende hadi katika ngazi ya vitongoji. “Tuendelee kuwa pamoja na kuja kwangu hapa nikuhakikishie tunaendelea kukupa ushirikiano.”

Waziri Mkuu Majaliwa na Mhashamu Askofu Pisa wakiwa katika mazungumzo kwenye makazi ya Askofu mkoani Lindi.
------------------------------------------

Kwa upande wake Askofu Pisa amemshukuru Rais Dkt Samia kwa salamu za pongezi za kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa TEC.

Uchaguzi wa viongozi wapya wa TEC uliohusisha nafasi za Rais, Makamu wa Rais na Katibu, ulifanyika Juni 21, 2024.

Waliochaguliwa ni Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa (Rais), Mhashamu Askofu Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda (Makamu wa Rais) na Padre Charles Kitima wa Jimbo Katoliki la Singida (Katibu Mkuu).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages