
Wanafunzi wa UDSM waliopata ufadhili wa kwenda kusoma nchini Afrika ya Kusini wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Barrick na chuo hicho
Dar es Salaam
---------------------
Kampuni ya Barrick nchini inayoendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals, imewafadhili wanafunzi watano kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenda kusoma shahada ya kwanza ya Elimu ya Madini na Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg ,Afrika ya Kusini kupitia progamu yake ya kuwezesha wasomi vijana inayotekelezwa Kanda ya Afrika na Mashariki ya kati.
Akizungumza katika hafla ya kutangaza ufadhili huo na kuwaaga wanafunzi waliofanikiwa kupata fursa hiyo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, alisema ufadhili huo ni ushuhuda na uthibitisho kwamba Barrick imelenga kukuza sekta ya madini kupitia uwekezaji wake, sambamba na kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Uwajibikaji wetu hauishii kuendesha migodi yetu kwa viwango vya kimataifa, bali pia tumejikita kuhakikisha tunawekeza katika kuwapatia Watanzania ujuzi, hususan kwa vijana ambao watakuwa wataalamu wa siku za usoni, ndio maana kupitia udhamini wa elimu kama huu kunawezesha kuwa na wataalamu wa fani ya madini na wabunifu watakaochangia kuleta maendeleo katika siku za usoni,” alisema Dkt. Ngido.

Dkt. Ngido alisema Barrick itakuwa karibu na wanafunzi hao, na pindi wakapomaliza masomo yao watapatiwa fursa ya kuwajengea uwezo wa kupata ujuzi zaidi kwa kuwapatia ajira katika migodi yake nchini.
Aliongeza kuwa dhamira ya kampuni ya Barrick ni kuendelea na ushirikiano wenye tija kwa kufanya uwekezaji endelevu wenye tija kwa Tanzania na watu wake - kwa kuhakikisha kwamba katika programu hiyo taifa linaweza kupata wataalamu mbalimbali kwenye fani ya uinjinia wa madini na jiolojia.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Ngido alifafanua kuwa kupitia programu hiyo, Barrick kwa kushirikiana na UDSM wataendelea kuhakikisha wanazalisha wataalamu wapya kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, aliIshukuru Barrick kuwapa ufadhili wanafunzi hao baada ya kushindanishwa na wenzao kutoka vyuo vikuu vingine hapa nchini.
“Tumefurahi na ufadhili huu na ni imani yangu watakwenda kusoma kwa bidhii na hakuna atakayerudishwa kwa kushindwa masomo, nawataka muwe mabalozi wazuri kwa chuo chetu na nchi kwa ujumla,” alisema Prof. Anangisye.
Alisema ufadhili kwa wanafunzi hao umetolewa baada ya mchujo wa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini na hatimaye hao wameshinda. “Hawa ni kati ya wanafunzi bora waliopita kwenye mchujo na kupata ufadhili kwenda kusoma shahada ya kwanza kwenye madini,” alisema.
“Ni furaha yangu kuona kwamba kati ya wanafunzi hawa waliopata ufadhili kuna wasichana, hii ni moja ya sera ya pale Mlimani kuweka uwiano wa jinsia kwenye masomo ili kuhakikisha watoto wa kike na wenye uwezo wanapata fursa za kusonga mbele,” alisisitiza Prof. Anangisye.

Mmoja ya wanafunzi hao akiongea kwa niaba ya wenzake, Samson Abeid, alisema programu hiyo ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wa kitanzania kwa kusoma kwa bidii na kuhakikisha kwamba wanatoa mchango katika maendeleo ya taifa.
“Programu hii itachochea chachu katika sekta ya elimu hapa nchini na kutoa fursa kwa wanafunzi wa kitanzania kupata elimu, maarifa na ujuzi nje ya nchini,” alisema Abeid.
No comments:
Post a Comment