NEWS

Wednesday 3 July 2024

Waziri Kairuki amshukuru Mwekezaji wa Grumeti Reserves kwa kusaidia uhifadhi, kupambana na ujangiliWaziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (kushoto) na Mwekezaji wa Grumeti Reserves Ltd, Paul Jones walipokutana jijini Dar es Salaam jana.
-----------------------------------------------

Na Happiness Shayo, Dar es Salaam
-----------------------------------------------

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Mwekezaji wa Pori la Akiba Grumeti (Grumeti Reserves), Paul Jones, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na uhifadhi na utalii.

Pori hilo liko katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, jana Julai 2,2024.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki ameishukuru Kampuni ya Grumeti Reserves Ltd kwa namna ambavyo imeendelea kujitolea katika shughuli mbalimbali za uhifadhi na utalii, na kuihamasisha kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Tunashukuru kwa misaada yenu katika uhifadhi na kupambana na ujangili, lakini tunaomba msaada katika ununuzi wa vifaa zaidi kwa ajili ya Askari wa Vijiji (Village Game Scouts) ili tuweze kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na vifaa vya mawasiliano na ununuzi wa mabomu ya pilipili,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Aidha, alisema yuko tayari kushirikiana na Kampuni ya Grumeti Reserves katika kukabiliana na changamoto ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika maeneo yao.

"Tuko tayari kutoa ushirikiano katika suala hili la ujenzi wa uzio katika eneo lenu, lakini muhimu mtoe elimu na kushirikisha wananchi ili wajue haki zao za msingi, wajue wanatoa nini na watafaidikaje," alisema.

Waziri Kairuki (katikati mwenye suti ya bluu), Mwekezaji Paul Jones (wa tano kushoto) na viongozi wengine mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Ultalii, TANAPA, TAWA na Grumeti Reserves wakiwa katika picha ya pamoja jijini Dar es Salaam jana.
-------------------------------------------------

Waziri Kairuki alitumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya uwekezaji ikijumuisha Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA) manne katika Pori la Akiba la Selous, Rungwa na Inyonga, na maeneo mengine.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alimtaka mwekezaji huyo kuendelea kutoa misaada kwa jamii inayozunguka eneo lake la uhifadhi, kuelimisha wananchi juu ya faida zitokanazo na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki, pamoja na ufugaji nyuki ili kuongeza uzalishaji wa asali nchini, ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan anayeweka mkazo juu ya ufugaji wa nyuki, hasa kwenye kuongeza mnyororo wa thamani.

Naye Mwekezaji wa Pori la Akiba Grumeti, Paul Jones aliiomba serikali kutoa ushirikiano endelevu katika mchakato wa kujenga uzio katika eneo la Pori la Akiba Grumeti, ili kukabiliana na changamoto ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Pia, alipongeza na kushukuru kwa ushirikiano uliopo kati ya Grumeti Reserves na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kwa upande wake Kamishna Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi aliwataka wawekezaji hao kushirikisha wadau wote wa uhifadhi wanapotaka kujenga uzio, wakiwemo wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Hassan Abbasi, Kamishna Uhifadhi wa TAWA na Maafisa Waandamizi kutoka TANAPA, TAWA na Grumeti Reserves Ltd.

Grumeti Reserves ni kampuni ya utalii wa kiikolojia ambayo inasaidia uhifadhi na maendeleo ya jamii katika mfumo ikolojia wa Serengeti, na imetengeneza ajira kwa mamia ya wananchi wa eneo hilo - wanaume na wanawake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages