
Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa.
-----------------------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------
Kampuni za madini zimechangia shilingi bilioni 96.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii nchini kati ya mwaka 2018 na 2023.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, mchango huo bado unaweza kuongezeka ikiwa changamoto zilizopo zitashughulikiwa ipasavyo, lakini pia ushirikiano kati ya kampuni na jamii utaimarishwa.
Dkt Kiruswa amesema Wizara ya Madini inaendelea kuhamasisha kampuni za madini kuongeza michango yao kwa jamii kupitia miradi ya CSR na kwamba kwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2023.
Aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha maboresho ya kanuni hizo, kilichofanyika jijini Dodoma jana Agosti 15, 2024.

Kwa upande mwingine, alisema Maboresho ya Kanuni na Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii (CSR) za Mwaka 2023 yamelenga kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa pamoja kati ya jamii na kampuni za madini katika utekelezaji wa miradi ya jamii.
Dkt Kiruswa alisema ushirikishwaji wa pamoja kati ya jamii na kampuni za madini ni jambo muhimu kwa maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka migodi.
Washiriki wa kikao hicho ni wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa leseni (kampuni za uchimbaji), wataalamu kutoka halmshauri ambako shughuli za madini zinafanyika kwa wingi nchini.
Wengine ni wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri ambako shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika, taasisi za umma, vyama vya wachimbaji na asasi za kiraia.
Dkt Kiruswa alisema kuwa tangu mwaka 2017, baada ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kufanyiwa marekebisho na kuongezwa kifungu cha 105 kinachohusu wajibu wa kampuni kwa jamii, mafanikio makubwa yameonekana sekta ya madini.
Licha ya mafanikio hayo, utekelezaji wa kanuni za CSR umekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitaji kushughulikiwa kupitia maboresho.
"Changamoto hizo ni pamoja na mipango ya miradi ya CSR kutoandaliwa kwa wakati na iliyoandaliwa kutotekelezwa kwa wakati, kukosekana kwa miongozo ya utekelezaji wa mipango ya CSR ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kuandaliwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuwashirikisha wamiliki wa leseni za madini,” alisema Dkt Kiruswa.
Alitaja changamoto zingine kuwa ni kupishana kwa mitazamo kati ya halmashauri na wamiliki wa leseni za madini kuhusiana na aina ya miradi na namna ya kuitekeleza na uelewa mdogo wa masuala ya CSR kwa jamii.
Pia, migogoro baina ya wamiliki wa leseni za madini na mamlaka za serikali za mitaa, hali inayosababisha baadhi ya miradi ya kijamii kutokukidhi mahitaji na matarajio ya jamii zinazozunguka migodi.
Kwa upande wake Kamishna wa Madini, Dkt AbdulRahman Mwanga alisema kikao hicho kinatambuliwa na Sheria ya Madini.
“Tunapofanya uvunaji wa madini, tunaona tuwe na utaratibu wa kurejesha kwa jamii ili kujenga mahusiano mazuri na kulinda biashara na shughuli za madini zifanyike vizuri, wizara inaona ni vizuri kupokea maoni ili kuboresha kanuni hizi,” alisema Mwanga.
Aliongeza kuwa maoni ya kikao hicho yatasaidia kupunguza changamoto zilizopo na kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuleta manufaa kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment