
Zao la tumbaku shambani
-----------------------------------
NA CHRISTOPHER GAMAINA
--------------------------------------------
Wakulima wa tumbaku na wataalamu wa kilimo katika wilaya ya Serengeti wamekitaja Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kama mkombozi wao, anayehuisha na kuendeleza kilimo cha zao hilo kilichokuwa mbioni kufutika kwenye ardhi ya wilaya hiyo.
Kwamba tangu chama hicho kiingie wilayani humo miaka miwili iliyopita, kimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa tumbaku katika usambazaji wa huduma za pembejeo na elimu ya kilimo bora cha zao hilo la biashara kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).
“Mfano, wanachama wa AMCOS yangu ya Ngarawani kwa sasa wanafanya vizuri sana katika kilimo cha tumbaku baada ya kuanza kupata mbolea na mafunzo kutoka WAMACU,” alisema Afisa Kilimo, Shida Jackson katika mahojiano na gazeti hili mjini Tarime jana.
Shida ni miongoni mwa maafisa kilimo na wakulima kutoka wilayani Serengeti wanaoshiriki mafunzo ya siku saba kuhusu kilimo bora cha tumbaku - yanyoendelea mjini Tarime chini ya uwezesho wa WAMACU Ltd.
“WAMACU pia wanafanya kazi kubwa ya kuimarisha AMCOS za wilayani Serengeti kwa kuzijengea uwezo wa kujiendesha na kuhudumia wakulima,” anasema Afisa Kilimo, Morris John kutoka Serengeti.
Kwa mujibu wa Mkulima Bung’ate Ryoba Marwa kutoka AMCOS ya Chapa Kazi, WAMACU pia imekuwa ikitetea wakulima wa tumbaku wasinyonywe na wanunuzi kwa kupunjwa bei ya zao hilo.
“Hakika tunajivunia hatua hii ya kujiunga na kushirikiana na WAMACU kwani ni chama cha ushirika chenye huduma ambazo ni rafiki kwa wakulima,” anasema mkulima wa tumbaku, Pius Mwita kutoka AMCOS ya Ngarawani.
Wakulima na maafisa kilimo wanaopata mafunzo ya mbinu za kilimo bora cha tumbaku wameonesha shauku ya kwenda kushawishi AMCOS za wilayani Serengeti ambazo hazijajiunga na WAMACU kufanya uamuzi wa kujiunga ili nazo ziweze kunufaika na huduma mbalimbali zikiwemo za pembejeo.
“Tutakwenda kuzieleza AMCOS zilizobaki umuhimu wa kujiunga na WAMACU, maana kwa hakika mkulima ukiwa nje ya ushirika huu unakosa vitu vingi muhimu kama haya mafunzo tunayopata,” anasema Afisa Kilimo, Morris John.
Dhamira ya chama hicho cha ushirika ni kuhakikisha wakulima wengi wanachangamkia kilimo cha tumbaku na hata mazao mengine ili kukuza kipato chao, kuinua uchumi wao, na hivyo kuboresha hali ya maisha yao.
WAMACU Ltd wamewezesha na kuratibu mafunzo hayo ya kilimo bora cha tumbaku kwa maofisa ugani/kilimo na watendaji wa AMCOS wakiwemo wakulima kutoka wilaya zinazolima zao hilo mkoani Mara.
Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) kuwajengea washiriki hao uelewa juu ya uendeshaji wa kilimo bora cha zao hilo la biashara.
Baada ya hapo wahitimu watakwenda kueneza mafunzo hayo kwa wakulima husika katika maeneo wanakotoka.
“Lengo la mafunzo haya ni kuhamasisha kilimo bora cha tumbaku na chenye tija ili kuinua kipato cha mkulima, halmashauri husika na kuiingizia nchi fedha za kigeni,” anasema Mtafiti Eric Zawadi kutoka TORITA.
Kwa mujibu wa Nasibu Salum Ngamba kutoka Kampuni ya Alliance One inayojihusisha na ununuzi wa tumbaku, mafunzo hayo yatawezesha wakulima wa zao hilo kuondoka kwenye kilimo cha mazoea kwenda kilimo biashara chenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo pia jukumu la kwenda kusimamia ubora wa zao la tumbaku kuanzia shambani hadi sokoni ili kuliwezesha kupata bei nzuri.
“Mkitoka hapa muende kuhamasisha wakulima zaidi kuitikia kilimo bora cha tumbaku ili kuinua pato lao, sambamba na kuwahimiza kujiunga na vyama vya ushirika waweze kuhudumiwa kwa urahisi,” alisema Surumbu wakati akifungua mafunzo hayo Agosti 13, mwaka huu.
Aidha, Surumbu amezielekeza kamati za kilimo za wilaya kuimarisha vikosi kazi vya kusimamia biashara ya mazao ya kimkakati, likiwemo la tumbaku katika maeneo yao ili kudhibiti utoroshaji wake na upotevu wa mapato ya serikali yatokanayo na ushuru wa mazao.
Alitumia nafasi hiyo pia kutuma wito kwa wakurugenzi watendaji na wakuu wa sekta ya kilimo katika maeneo yanayozalisha tumbaku na mazao mengine ya kimkakati kujitahidi kutenga bajeti ya kutosha kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao na ukusanyaji wa mapato.
Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye alisema ushirika huo unaunganisha wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kahawa na tumbaku kutoka wilaya za Tarime, Serengeti, Butiama, Rorya na Buchosa.
Gisiboye alibainisha kuwa lengo la WAMACU ni kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama wake - kwa kuhamasisha, kuongeza na kuimarisha uzalishaji wenye tija, kukusanya, kuhifadhi, kusindika na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi yenye tija kwa wakulima.
“Pia, WAMACU turatibu upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa maslahi ya wakulima, kuimarisha uwezo wa vyama na wanachama katika kutoa huduma zenye tija kwa wakulima, sambamba na kutafuta na kusogeza huduma ya pembejeo za kilimo karibu na wakulima,” aliongeza.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mafunzo hayo ni pamoja na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mara, Lucas Kiondore, Mwenyekiti wa WAMACU Ltd, Momanyi Range na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye.
No comments:
Post a Comment