
Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Shirika la EMEDO la jijini Mwanza limeahidi kuipatia Shule ya Msingi Sweya msaada wa mashine ya kurudufu (photocopy machine) kubwa ili kuitatulia changamoto ya gharama za kurudufu mitihani ya wanafunzi.
Mjumbe wa Bodi ya EMEDO, Edwin Soko aliyemwakilisha Mkurugenzi wa shirika hilo, Edutruth Lukanga wakati wa mahafali ya wahitimu wa darasa la saba shuleni hapo jana, alisema watatoa mashine hiyo ili wanafunzi waweze kupata mitihani kwa wakati.
"EMEDO tumeguswa na ombi lenu na sasa tutatoa mashine hiyo, na jukumu lenu kubwa iwe ni kuitunza ili iwasaidie kwa muda mrefu," alisema Soko.
Aidha, alisema EMEDO wanaendelea na jitihada za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya shule mbalimbali, ambapo Sweya ni moja ya shule nufaika kwenye uwezeshwaji wa utunzaji wa mazingira, na aliwataka waendelee kuwa mabalozi wazuri wa utunzaji wa mazingira.

Soko aliongeza kuwa EMEDO inatekeleza mradi wa kuzuia kuzama maji kwa kutoa elimu na vifaa mbalimbali vya kujikinga kwenye maeneo mbalimbali katika Kanda ya Ziwa, na hivyo kuwataka wazazi kuwa mabalozi wazuri kwani kuzama maji kunazuilika.
Pia, hakusita kuipongeza shule hiyo kwa kufanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba mwaka 2024, ambapo wanafunzi wote 92 waliohitimu walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari.

Katika mahafali hayo, wahitimu zaidi ya 102 waliohitimu darasa la saba mwaka 2024 walipewa vyetu vyao vya kuhitimu elimu ya msingi.
Shule ya Msingi Sweya ipo kata ya Luchelele, wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza na kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 800.
No comments:
Post a Comment