Kada maarufu wa CCM, Nyambari Nyangwine (mwenye kofia nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na makada mbalimbali alipotembelea ofisi za CCM Wilaya ya Tarime leo asubuhi. Kushoto kwake ni Katibu wa Wilaya, Noverty Kibaji na kulia kwake ni Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard.
-------------------------------------------------
Tarime
Kada maarufu wa chama tawala - CCM, Nyambari Nyangwine amesema yuko tayari kushirikiana na chama hicho wilaya ya Tarime, mkoani Mara ili kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo katika chaguzi zijazo.
Nyambari ambaye pia ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, ametoa kauli hiyo alipotembelea ofisi za CCM Wilaya ya Tarime na kuzungumza na viongozi wake leo asubuhi.
"Niko tayari kuendelea kuunga mkono CCM Tarime hata katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa," Nyambari amemwahidi Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji katika mazungumzo yao.
Nyambari Nyangwine akisaini kwenye kitabu cha wageni katika ofisi za CCM Wilaya ya Tarime.
--------------------------------------------
Kwa upande wake Katibu Kibaji amemshukuru Nyambari kwa kuona umuhimu wa kutembelea ofisi za chama hicho huku akimtaja kama kada mstaarabu anayekiheshimisha chama hicho tawala.
"Nikushukuru kwa kututembelea, nimekuwa nakusikia lakini leo nimekuona live (mubashara). Katika watu walioweka ustarabu ni pamoja na wewe. Nikuombe uendelee kukiheshimisha chama," Kibaji amemwambia Nyambari.
Katibu huyo ametumia nafasi hiyo pia kutuma wito wa kuwakumbusha wazaliwa wa Tarime walio nje ya wilaya hiyo kuiga mfano wa Nyambari kwa kukumbuka kurudi kuendeleza nguvu za kukijenga CCM kwa maendeleo ya wananchi.
Nyambari Nyangwine alipata kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010 hadi 2015 kwa tiketi ya CCM.
No comments:
Post a Comment