Moja ya mitaa ya mji wa Mugumu
----------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Serengeti
Umeyeyuka. Ndivyo tunavyoweza kuelezea mradi wa kuubadilisha mji wa Mugumu kuwa wa kisasa na kujulikana kwa jina la Serengeti Smart City - ambao kwa sasa umezungukwa na wimbi kubwa la sintofahamu.
Mugumu ndiyo makao makuu ya wilaya ya Serengeti ambayo eneo lake kubwa linatumika kwa uhifadhi wa wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii barani Afrika.
Mamlaka za wilaya hiyo zimekuwa zikitangaza na kuwapa wananchi matumaini ya Serengeti Smart City zikisema ni mradi mkubwa wa kimkakati uliopangwa kuhusisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Serengeti hadi jijini Mwanza, uboreshaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa miradi iliyokwama kwa muda mrefu, ukiwemo uwanja wa ndege Mugumu uliokwama kwa miaka miaka takriban 18 sasa.
Ujenzi wa mradi wa Serengeti Smart City ulitangazwa Februari 8, 2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo wakati huo, Dkt Vincent Mashinji.
Dkt Mashinji ambaye alimemishiwa wilayani Manyoni miezi michache iliyopita, alisema katika kikao hicho kwamba serikali imetoa shilingi zaidi ya trilioni mbili kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa miundombinu itakayoubadilisha mji wa Mugumu kuwa Serengeti Smart City.
“Tulianzisha andiko la mradi wa Serengeti Smart City, serikali imekubali, tayari zaidi ya trilioni mbili zipo tayari kujenga mji wa kisasa Serengeti, utakuwa ni mradi shirikishi kati ya serikali na wananchi.
“Tayari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti [Afraha Hassan wa wakati huo] ameitwa Dodoma kwenda kujadili ujenzi wa uwanja wa ndege Serengeti, na asilimia 30 ya fedha hizo [za ujenzi] zitaenda kwenye kampuni za wazawa,” alisema Dkt Mashinji.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Sauti ya Mara wilayani Serengeti wiki iliyopita unaonesha hakuna taarifa zinazothibitisha uwepo wa mradi huo.
“Ni kama stori zisizokuwa na matumaini kwa maendeleo ya Serengeti na watu wake. Suala la Serengeti Smart City lilikuwa kwenye mabano… ilikuwa ni ajenda ya kiongozi mmoja,” alisema Diwani wa Kata ya Morotonga, Musa Magasi.
Naye Diwani wa Kata ya Ikoma, Michael Machaba Kunani alisema mpango wa wa mradi huo haukuwahi kuwasilishwa kwenye kikao chochote cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Kwa upande wake Mwenyekit wa chama tawala - CCM Wilaya ya Serengeti, Mrobanda Japan alisema hafahamu chochote kuhusu mradi wa Serengeti Smart City.
Taarifa zaidi kutoka kwenye vyanzo vyetu inasema mradi huo haujwahi kupitishwa au kujadiliwa katika vikao halali vya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“Huu ni kama mradi hewa, hakuna hata sehemu moja mradi huu umewahi kujadiliwa na vikao vya madiwani wa Halmashauri ya Serengeti, haupo kwenye mhutasari wowote,” kilitokeza chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
No comments:
Post a Comment