NEWS

Saturday 28 September 2024

AICT, Right to Play wahamasisha elimu kwa mtoto wa kike Nyanungu



Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kegonga wilayani Tarime akipokea zawadi ya jezi kwa niaba ya timu yake ya mpira wa pete wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT kwa kushirikiana na Right to Play jana Septemba 27, 2024.
---------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News
Tarime

Wananchi wa vijiji vya Kegonga na Nyandage vilivyopo kata ya Nyanungu wilayani Tarime, Mara wamehamasishwa kuzingatia haki ya elimu kwa watoto wa kike, sambamba na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

Hamasa hiyo ilitolewa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi Kegoga na Nyandage, lililoandaliwa na taasisi hizo na kufanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kegonga jana Septemba27, 2024.

Afisa Mradi kutoka AICT na Right to Play, Daniel Fungo alisema lengo la tamasha hilo lilikuwa kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili waweze kutimiza ndoto za kielimu.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyandage 
wakicheza igizo wakati wa tamasha hilo.
-------------------------------------------------

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kegonga, Moses Michael Mkwalakwala aliwashukuru AICT na Right to Play kwa kufikisha elimu na hamasa hiyo katani Nyanungu.

"Nitoe shukrani za dhati kwa AICT na Right to play kwa kutuletea elimu hii, Nitoe wito kwa jamii kuhakikisha kwamba kila mtoto wa kike anapelekwa shule kwa manufaa yao na jamii," alisema Mwalimu Mkwalakwala.

Nao wenyeviti wa kamati za shule za Kegonga na Nyandage walitoa witoa kwa jamii kushirikiana na walimu kwa karibu ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wowote.

Tamasha hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu kwa wavulana na mpira wa pete kwa wasichana, kwaya na maigizo yenye jumbe mbalimbali za kukemea ukatili wa kijinsia, na kuelimisha jamii umuhimu kuwapa watoto wa kike na kiume fursa sawa ya elimu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages