NEWS

Wednesday, 6 November 2024

Sekondari 11 Tarime Mji zanufaika na msaada wa vitabu kutoka Nyambari Nyangwine Foundation



Msemaji wa Nyambari Nyangwine Foundation, Jacob Mugini akikabidhi msaada wa vitabu uliotolewa na taasisi hiyo kwa Shule ya Sekondari mpya Gicheri jana.
------------------------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News

Shule za sekondari 11, zikiwemo mbili mpya zilizojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, zimepokea msaada wa vitabu vya kiada na ziada vyenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 22 kutoka Taasisi ya Nyambari Nyangwine (NNF).

Sekondari zilizogawiwa msaada huo wa vitabu juzi na jana ni Ikoro (mpya), Gicheri (mpya), Nyamisangura, Iganana, Bomani, Rebu, Turwa, Angel House, Tagota, Kenyamanyori na Nkende.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Turwa wakifurahia msaada wa vitabu kutoka Nyambari Nyangwine Foundation.
----------------------------------------------

Akikabidhi vitabu hivyo kwa nyakati tofauti, Msemaji wa NNF, Jacob Mugini alisema taasisi hiyo imetoa msaada huo baada ya kuombwa na shule hizo na wadau wa elimu, ili kuzipunguzia mahitaji makubwa wa vitabu.

Walimu na wanafunzi wa shule hizo waliishukuru Taasisi ya Nyambari Nyangwine wakisema msaada wa vitabu hivyo utachochea maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi.


Makabidhiano ya msaada wa vitabu katika Shule ya Sekondari Kenyamanyori.
------------------------------------------------

“Mungu ni mwema, mmepunguza presha kwa mlichokileta, tulikuwa tukiwaza mwaka kesho tutafanyaje. Mama [Rais Dkt Samia Suluhu Hassan] kajenga majengo, vitabu vimepatikana - vitasaidia wanafunzi kusoma na kutimiza ndoto zao,” Mkuu wa Shule ya Sekondari Ikoro, Mwalimu Lilyan Onea alisema.

Mkuu wa Sekondari Gicheri, Mwalimu Led Pius naye aliishukuru Taasisi ya Nyambari Nyangwine akisema msaada wa vitabu hivyo una maana kubwa kwa shule hiyo mpya.


Makabidhiano ya msaada wa vitabu katika Shule ya Sekondari Tagota.
-------------------------------------------------

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kenyamanyori, Mwalimu Chacha Nyaite alisema: “Shukurani kwa Nyambari Nyangwine Foundation, mfikishie salaamu, tunaahidi vitabu hivi vitakuwa chachu ya maendeleo ya kitaaluma.”

Nao wanafunzi wa shule hizo hawakusita kuonesha furaha yao na kuahidi kusoma kwa bidi.

“Tunashukuru kutuletea vitabu, tutajifunza kwa weledi kwa kushirikiana na walimu,” alisema Pili Wilbert, mwanafunzi wa sekondari ya Ikoro.


Makabidhiano ya msaada wa vitabu katika Shule ya Sekondari Turwa.
-------------------------------------------

Mwanafunzi mwingine, Jean Binagi alisema: “Tunashukuru sana kwa huu msaada wa vitabu kutoka Nyambari Nyangwine Foundation, tunaahidi kusoma vizuri na tutafaulu kwa division one na two.”


Makabidhiano ya msaada wa vitabu katika Shule ya Sekondari Ikoro.
------------------------------------------------

Nyambari Nyangwine Foundation ilianza rasmi shughuli ya ugawaji wa msaada wa vitabu kwenye shule za sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Tarime Novemba 4,2024.


Msemaji wa taasisi hiyo, Jacob Mugini aliambatana na baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo katika usambazaji wa msaada wa vitabu hivyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages