
Kampeni ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia ikiendelea kijijini Nyamwaga jana.
-------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Kampeni ya Siku 16 Kupinga Ukatili wa Kijinsia, ukiwemo ukeketaji sasa inafanyika kijiji kwa kijiji, kwa ufadhili wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ukishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Jana, kampeni hiyo ilifanyika katika kijiji cha Nyamwaga, kimojawapo cha vijiji 11 vilivo jirani na mgodi wa North Mara, ambapo wananchi wanapata elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia, na kwa upande mwingine uelewa wa masuala ya kisheria, kupitia kwa mawakili wa kujitegemea kutoka Kampuni ya BOWMANS.

Pichani ni mawakili wa kujitegemea (wa pili, wa tatu na wa nne kutoka kushoto), Afisa Maendeleo ya Jamii (kulia) na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyamwaga walioshiriki katika kampeni hiyo.
-----------------------------------
Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kunakuwepo na dhana ya usawa katika jamii na haki inatolewa kwa watu wa tabaka la chini ambao hawana uwezo wa kulipa gharama za mawakili katika masuala mbalimbali ya kisheria.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mussa Maulid Magope alitoa wito kuhamasisha wanavijiji kujitokeza kwa wingi kupata elimu na msaada wa kisheria kupitia kampeni hiyo.
"Natoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi ndani ya siku tano za kampeni hii katika vijijini 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara. Huduma hii ni bure, hakuna gharama yoyote,” alisema.
Kwa mujibu wa Magope, ni agizo na takwa la serikali la kuhakikisha kuwa huduma za msaada wa kisheria zinapatikana maeneo yote nchini.
Wakazi wa kijiji cha Nyamwaga walieleza kuridhishwa na elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, pamoja na huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa katika kampeni hiyo.

Mkazi wa kijiji cha Nyamwaga (kulia) akipata huduma ya msaada wa kisheria kutoka kwa mawakili.
-------------------------------
"Nimepokewa vizuri na nimepewa ufafanuzi zaidi. Nmefahamu kumbe hata sisi wanawake tuna haki ya kumiliki ardhi kama wanaume," alisema Sara Joseph Magoko.
Naye Patrick Ragita alisema: "Hii ni faraja kwetu wazee tusio na kipato cha kuwalipa mawakili kutusimamia kwenye kesi. Tunaomba huu mpango uwe endelevu ili watu wa chini wasinyanyasike."
Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ilizinduliwa Novemba 25, mwaka huu kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nyamongo kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Jeshi la Polisi na mgodi wa North Mara, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Meja Edward Flowin Gowele.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
No comments:
Post a Comment