
---------------------------------
MAAMBUKIZI ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanaweza kupungua zaidi katika jamii, ikiwa kutakuwepo na nguvu ya pamoja inayojumuisha Serikali, wadau wa kisekta na jamii nzima katika kukabiliana nayo.
Hayo yameelezwa leo Desemba 1, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyoratibiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kudhaminiwa na Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Maadhimisho hayo yamefanyika kiwilaya kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe na kuhutubiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele kama mgeni rasmi.
Katika hotuba yake, Mwalimu Mwaisenye amesema kwa sasa Serikali imetenga shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kukopesha vikundi mbalimbali kwenye maeneo yenye maambuki makubwa ya VVU wilayani Tarime.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye akimkabidhi mmoja wa wajasiriamali kitambulisho wakati wa maadhimisho hayo.
------------------------------
"Serikali imeweka mifumo ya uwezeshaji makundi haya kiuchumi, ambapo kwa Halmshauri ya Wilaya ya Tarime kuna fedha za mikopo shilingi bilioni 2.4 kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani," amesema.
Kwa upande wake Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko amesema ushirikiano katika kutoa elimu na kukemea unyanyapaa kwa waathirika ni nyenzo muhimu katika kupambana na VVU na Ukimwi.
"Uelewa wa UKIMWI ni jambo la msingi na hatua muhimu katika kuzuia maambukizi. Kwa pamoja tunaweza kuzuia maambukizi na unyanyapaa katika jamii.
"Sisi mgodi tumejitolea kuwa majirani na washirika wenu kusaidia jitihada za kuboresha maisha na kuimarisha jamii," amesema GM Lyambiko.
Mwanafunzi akiuliza swali wakati wa maadhimisho hayo.
------------------------------
Awali, Mratibu wa UKIMWI wa Wilaya ya Tarime, Godfrey Mkenda amesema maambukizi ya VVU katika wilaya hiyp yamepungua kutoka asilimia 1.7 mwaka 2023/2024 hadi asilimia 1.5 Novemba 2024.
Mkenda ametaja mikikati ya kukabiliana na tatizo hilo ni pamoja na elimu kwa jamii, mafunzo kwa watumishi, kuimarisha upimaji wa VVU na kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya tiba, ushauri nasaha na kuhamasisha matumizi ya dawa za kufubaza virusi hivyo.
Maadhimisho hayo yamefanyika sambamba na utoaji wa elimu na huduma mbalimbali za afya, zikiwemo za upimaji wa VVU na ugawaji wa kondomu bila malipo.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu wa 2024 inasema: “Chagua Njia Sahihi Tokomeza Ukimwi”.
No comments:
Post a Comment