NEWS

Friday, 29 November 2024

CCM Musoma Vijijini yashinda kwa kishindo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa




Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Chama tawala - CCM Musoma Vijijini kimepata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, baada ya kupata asilimia 97.06 ya kura zote zilizopigwa katika vijiji vyote 68 vya jimbo hilo.

Kwa upande wake chama cha upinzani - CHADEMA kimeambulia asilimia 2.94 zilizobaki baada ya kupata ushindi kwenye vijiji viwili katika uchaguzi huo uliofanyika juzi Novemba 27, 2024.

Jimbo la Musoma Vijijini lina kata 21, vijiji 68 na vitongoji 374.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Prof Sospeter Muhongo ilieleza kwamba CCM pia ilijizolea asilimia 95.45 ya nafasi za uongozi katika vitongoji 357, ikilinganishwa na asilimia 4.55 zilizokwenda CHADEMA.

Katika taarifa yake kwa wapiga kura wa jimbo hilo, Prof Muhongo alisema: "Tusisahau kwamba sisi Musoma Vijijini huwa hatuna ubaguzi wa kisiasa wala wa aina yoyote ile."

"Muhimu kwetu ni maendeleo shirikishi kwa manufaa ya jamii yote ndani ya vitongoji, vijiji na kata zetu zote," aliongeza Prof Muhongo.

Mbunge wa Musoma Jimbo la Vijijini, 
Profesa Sospeter Muhongo.

Taarifa ya mbunge huyo ambayo ilijaa hamasa ya maendeleo kwa wananchi, iliongeza kuwa kuanzia wiki ijayo "tutaendelea na utekelezaji wa miradi yetu iliyobuniwa na kuanza kutekelezwa kwa kutumia nguvu za wavijijji".

Baadhi ya miradi hiyo imeanza kupata michango ya fedha kutoka serikalini, kwa mujibu wa Prof Muhongo.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi kwa kila sekondari ya kata, sekondari mpya 10, shule shikizi nane na zahanati 17.

Jimbo la Musoma Vijijini limepata sifa kubwa ya kutekeleza miradi mingi ya sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya barabara.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages