
Mkurugenzi wa Kampuni ya Nice Construction and General Supplies Ltd, Lameck Airo akimwonesha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi sehemu ya eneo linakojengwa Soko la Mazao Sirari, wilayani Tarime jana Jumatatu.
-------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, jana Jumatatu alikagua maendeleo ya ukamilishaji wa ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao Sirari lililopo wilayani Tarime, mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kiongozi huyo wa mkoa amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa kimkakati kuukamilisha kwa wakati.
”Ninakujua wewe ni mkandarasi mwenye uwezo, kamilisha ujenzi huu kwa wakati,” Kanali Mtambi alimwambia Lameck Airo, Mkurugenzi wa kampuni inayotekeleza mradi huo ya Nice Construction and General Supplies Ltd yenye makao makuu jijini Mwanza.
Picha zote na Mara Online News
Awali, akiwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa taarifa fupi ya ukamilishaji wa ujenzi wa soko hilo, Mkurugenzi wa Ufundi wa kampuni hiyo alisema utekelezaji huo ulianza rasmi Novemba 28, mwaka jana na unatarajiwa kukamilishwa Mei 28, mwaka huu.
Alibainisha kuwa ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.046 kutoka serikalini, umefikia asilimia 60.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Kanali Mtambi aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Gerald Musabila Kusaya, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Flowin Gowele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, miongoni mwa viongozi wengine.
No comments:
Post a Comment