NEWS

Saturday, 1 February 2025

Tarime Vijijini: Nyambari awatua mzigo wazazi wa wanafunzi Shule ya Msingi Mangucha



Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine, Sospeter Migera Paul (aliyevaa fulana ya bluu) akikabidhi msaada wa photocopy machine na printer mpya katika Shule ya Msingi Mangucha uliyopo kata ya Nyanungu, wilayani Tarime jana Januari 31, 2025. (Picha na Mara Online News)
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mangucha iliyopo kata ya Nyanungu, wilayani Tarime wamemshukuru Nyambari Nyangwine kwa kuwatua mzigo wa michango ya fedha za kudurufu na kuprinti karatasi za mitihani, baada ya kuipatia shule hiyo msaada wa photocopy machine na printer mpya.

“Tunamshukuru sana Mhesimiwa Nyambari Nyangwine kwa msaada huu muhimu, sisi wananchi wa kijiji cha Mangucha tunaendelea kutambua na kuthamini michango yake mbalimbali ya kimaendeleo tangu akiwa Mbunge wa Jimbo la Tarime,” alisema Gideon Ngicha Mnyoro, mkazi wa kijiji cha Mangucha na Katibu wa CCM Tawi la Mangucha.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Mangucha, Mseti Tembo akizungumza wakati wa mapokezi ya msaada wa vifaa hivyo shuleni hapo jana Januari 31, 2025 aliwaomba walimu na wanafunzi kuvitunza vizuri ili vidumu muda mrefu.

Akikabidhi msaada wa vifaa hivyo, Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine, Sospeter Migera Paul alisema Nyambari ambaye alisoma katika Shule ya Msingi Mangucha hakuona sababu ya kusita kutoa msaada huo baada ya kuombwa na uongozi wa shule hiyo wakati wa mahafali ya darasa la saba mwaka jana.

Migera alifafanua kuwa Nyambari ameona fahari kuipatia shule hiyo msaada wa mashine za kudurufu na kuprinti mitihani ya wanafunzi ili kuwaondolea wazazi na walezi usumbufu wa kuchangishwa fedha.

Inaelezwa kuwa shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1957, imetoa viongozi na watu wengi maarufu nchini, akiwemo Nyambari ambaye kwa sasa anatajwa kuwa mmoja wa wawekezaji wazawa ambao wameanza kuwekeza nje ya mipaka ya Tanzania.

Baadhi ya mataifa mabayo Nyambari ameanza kuwekeza ni Uganda na DR Congo.

Nyambari Nyangwine ni mfanyabiashara, mchapishaji na mwandishi maarufu wa vitabu nchini, na aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010-2015 kwa tiketi ya chama tawala - CCM.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages