NEWS

Wednesday, 30 April 2025

Meja Gowele awa Mkuu wa Wilaya wa kwanza kutangaza Mlima Tarime kivutio cha utalii



Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Flowin Gowele, akiwa juu ya Mlima Tarime.
------------------------------------

Na Christopher Gamaina

Huenda Mlima Tarime ukaingia kwenye orodha ya vivutio vikubwa vya utalii mkoani Mara, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele, kuutembelea na kukubaliana na wazee wa mila kuulinda kimazingira na kiusalama.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya wilaya hiyo, kiongozi huyo alipanda kwa miguu hadi kilele cha mlima huo uliopo nje kidogo ya mji wa Tarime, akiongozana na wataalamu wa mazingira, ardhi, misitu na uhifadhi.

Meja Gowele ambaye anatajwa kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza kupanda mlima huo, alikutana na wazee wa mila, baadhi ya viongozi na wakazi wa mitaa husika, akaoneshwa na kuelezwa maajabu ya hazina ya asili inayopatikana juu ya mlima huo.

Miongoni mwa maajabu hayo ni hifadhi ya miti ya asili inayoaminika kuwa na uwezo wa kuzuia vurugu na kuzima nguvu za silaha kwenye mapigano.

“Huu mti unaitwa Ikesenda - kiimani unasaidia kupunguza vurugu, na huu mwingine unaitwa Irikube ambao kiimani unazuia silaha za kivita zisifanye kazi. Miti hii ilipandwa na wazee wetu,” Katibu wa Baraza la Wazee wa Mila Butimbaru - Inchage, Mwita Nyasibora Matinde, alimueleza Meja Gowele na msafara wake huku akiwaonesha miti hiyo.

Alielezwa pia uwepo wa kisima cha asili kinachoitwa Boranga juu ya mlima huo kisichokauka maji. “Kisima hiki ndicho asili ya jina “Tarime” lenye maana ya “maji yasiyozimika,” alisema Nyasibora.

Zaidi ya hayo, alielezwa na kuoneshwa maeneo tofauti ya faragha yanayotumika kwa shughuli za matambiko ya kimila na ibada za kidini.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Koo ya Watimbaru, Charles Mwita Mbogo, alionesha umuhimu wa baraza hilo kuendelea kuhitaji ushirikiano na serikali katika jitihada za kuzuia shughuli za kilimo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira hai ya mlima huo.

Kwa Meja Gowele, kupanda mlima huo kwa miguu kulikuwa zaidi ya tukio la kawaida, ilikuwa ni safari ya kugundua uzuri uliojificha.

“Nimeona baraka sana leo, ukisimama hapa juu unaiona Tarime yote kwa wakati mmoja, na kwa kweli panapendeza sana, mimi sikujua kama Tarime yetu ni nzuri namna hii,” alisema kwa furaha.

Kutokana na hali hiyo, Meja Gowele alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuuhifadhi mlima huo, ikiwa ni pamoja na kupanda miti, hasa ya asili ili kudumisha uasili wake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Aliwapongeza wazee wa mila kwa jitihada zao za kuulinda mlima huo, akisema zinaunga mkono maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan na Makamu wake, Dkt Isdor Mpango, yanayomtaka kila mwananchi kushiriki kutunza mazingira.

Kwa msingi huo, Meja Gowele alitangaza kwamba kuanzia sasa Mlima Tarime utakuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayolengwa na shughuli za upandaji wa miti milioni 1.5 kila mwaka katika wilaya ya Tarime.

“Mbali na hifadhi ya serikali, milima inatumiwa na wazee wetu kwa ajili ya mambo ya mila, na mpaka watu wa dini nimeambiwa wanakuja kufanya ibada zao hapa, kwa hiyo lazima tuyatunze mazingira ya mlima huu.

“Lakini pia, mmeniambia asili ya neno Tarime ni kisima cha asili kilichopo hapa ambacho hakiishiwi maji, na ndio maana Tarime tunapata mvua nyingi kuliko maeneo mengine.

“Hii milima ndiyo inatuletea mvua, misitu inatusaidia kupata mvua, kwa hiyo wazee wangu leo nimekuja na watumishi husika kwa ajili ya kuweka mikakati ya kulinda na kuhifadhi mlima huu,” alisema Meja Gowele.

Aliahidi kuanzisha na kuongoza kampeni maalum ya kuulinda mlima huo, hususan kwa kupanda miti. “Tutapanda miti mvua ziendelee kuja Tarime ili hii maana ya neno Tarime kwamba ni maji yasiyokauka basi iendelee kudhihirika,” alisisitiza.

Kampeni hiyo itafanyika sambamba na kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi vitakavyopata mikopo kutoka Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa ajili ya kufuga nyuki ili kulinda mazingira ya mlima huo, lakini pia kuwapatia kipato kutokana na mavuno ya asali.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa ofisi yake imedhamiria kushirikiana na wazee wa mila katika suala zima la usimamia wa mlima huo. “Wazee mkisema jambo lazima tulisikilize na tuliheshimu, hakuna sehemu tutafanya kazi bila kuwasikiliza wazee,” aliwambia.

Aidha, mbali na shughuli za imani za kimila, ibada za kidini na mazingira yanayovutia utalii, Meja Gowele alisema mlima huo ni muhimu pia katika ulinzi wa usalama wa wilaya ya Tarime na wakazi wake.

“Kwa maana ya kiusalama, hapa ndipo usalama wa Tarime ulipo, vyombo vyetu vya usalama vitakuwa vinatembelea hapa mara kwa mara kuangalia usalama, ikiwa ni pamoja na kuhakiki watu wote, wakiwemo wanaotoka nje ya nchi kuja hapa kufanya ibada na matambiko.

“Katika hili, wenyeviti wa mitaa mhakikishe mnawatambua wote wanaokuja hapa ili baadhi yao wasije wakatumie nafasi hii vibaya, najua wazee wetu wa mila mtakuwa mnaangalia na hili pia,” alisema.

Kuhusu kilimo, Meja Gowele alielekeza kuwa shughuli hizo zifanyike maeneo ya chini kabisa ya Mlima Tarime na kusisitiza kwamba mtu yeyote hataruhusiwa kulima juu ya mlima huo.

Wataalamu wa ardhi na mazingira alioongozana nao walishauri kuwa hata maeneo ya katikati ya mlima huo hayatakiwi kulimwa kwani kuna majabali ya miamba ambayo kilimo kinaweza kumomonyoa udongo na kuyasababisha kuporomoka na kuleta madhara kwa watu.

Hivyo, mlima huo sasa unaingizwa rasmi kwenye mikakati ya makusudi ya kuufanya kuwa kivutio muhimu cha utalii katika wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

Kwa upanda mwingine, Mlima Tarime ni mojawapo ya sehemu za kufanyia mazoezi, kwani watu wanaoupanda lazima watoe jasho, hali ambayo inasaidia kuimarisha afya ya mwili, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

Lakini pia, mtu akiwa juu ya mlima huo anafurahia hewa nzuri ya asili ambayo kulingana na wataalamu wa saikolojia, inasaidia kupunguza kama si kuondoa kabisa msongo wa mawazo.

Ndio maana Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Flowin Gowele, amedhamiria kushirikiana na wazee wa mila kuulinda, kuuhifadhi na kuutangaza kwa umma, akisema: “Karibu Tarime kwa utalii wa kujionea maajabu ya kihistoria, imani na mandari ya kipekee katika Mlima Tarime”.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages