NEWS

Wednesday, 30 April 2025

Matunda ya CSR: Mgodi wa North Mara wazindua utekelezaji mwingine wa miradi ya barabara, maji



Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, viongozi wa kijamii, watumishi wa serikali, wadau na wakazi wa vijiji vinavyopakana na mgodi huo waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa miradi ya kijamii - iliyofanyika katika mji mdogo wa Nyamongo jana Jumanne.
------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) umezindua rasmi awamu nyingine ya utekelezaji wa miradi 19 ya barabara na mmoja wa maji katika vijiji 11 vilivyo Jirani nao.

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Uzinduzi wa utekelezaji wa miradi hiyo ulifanyika jana Jumanne katika mji mdogo wa Nyamongo na kuhudhuriwa pia na wadau mbalimbali, wakiwemo kutoka Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC).

Pia, tasisi muhimu za RUWASA na TARURA, viongozi wa serikali za vijiji hivyo na kata jirani, walishiriki katika hafla ya uzinduzi huo.

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mahusiano ya mgodi huo wa North Mara, Christopher Hermence, alitoa ufafanuzi jinsi miradi hiyo itakavyoanza kutekelezwa.

"Tukio la leo ni kuanza utekelezaji wa miradi ya barabara 19 na mmoja mkubwa wa maji. Kama jamii sasa tuwe na ushirikiano ili miradi hii iweze kutekelezwa kwa wakati.

"Kwa mfano, mradi wa maji utajumuisha uchimbaji wa mitaro kwenye baadhi ya maeneo, wananchi na viongozi muwape ushirikiano wakandarasi ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

"Kwa upande wa barabara pia kuna haja ya kutoa ushirikiano. Na ninyi wakandarasi kama kuna shughuli inatakiwa kufanyika na eneo fulani la mwananchi linaguswa tuhakikishe kuwa viongozi wanashirikishwa kabla ya kwenda kwenye eneo hilo ili kupungua malalamiko kutoka kwa wananchi," alisema Hermence.
 (Picha zote na Mara Online News)

Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mohamed Mtopa, alimtaka mkandarasi wa mradi huo wa maji kuhakikisha kuwa unakamilia kwa muda uliopangwa ili uanze kuhudumia wananchi.

Godfrey Kegoye, Diwani wa Kata ya Matongo ambako tayari mradi wa mkubwa wa maji umetekelezwa kwa ajili ya kuhudumia vijiji vine, alizishukuru mamlaka za serikali kwa kukubali utekelezaji wa miradi hiyo kutokana na fedha zinazotolewa na mgodi huo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

"Nishukuru Halmashauri ya Wilaya na mkoa kukubali kutenga pesa shilingi bilioni 2.5, kuboresha mradi wa maji katika kata ya Matongo na sasa katika vijiji vingine vilivyopo kata ya Kemambo utakaotekelezwa katika kijiji cha Kewanja.

"Tunashawishi wananchi kila mtu avute maji nyumbani kwake - maji yatakuwa mengi ya kutosha, tunaanza na lita laki moja - tenki lipo hapo mlimani, lakini pia tuna mpango wa kuweka tenki la lita laki tano kumaliza shida ya maji katika ukanda huu.

Kwa upande wake, mkazi wa Nyamongo, Rhobina Samson Mwita alisukuru akisema: "Kwa kweli naona Mungu amefungua njia, mradi tunaukubali na kuupokea mikono mwili, akina mama ndio wahanga wa maji na maji ndio uhai."

"Nimefurahi mradi kutufikia, wafanye bidii maji yatufikie kwa bei nnafuu," alisema mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mariamu Mwita Nega.

Naye Damian Makori ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu Nyamongo, aliunga mkono hatua hiyo ya mgodi wa North Mara akisema: "Nikiri wazi uwepo wa Barrick umesaidia mambo mengi, juzi tumeshuhudia madawati mengi yameletwa kwenye shule za watoto wetu, na leo tunashuhudia miradi ya maji na barabara."

"Tunahitaji ushirikiano pindi mradi unapoanza kutekelezwa kusiwepo ukwamishaji na migogoro pindi mkandarasi anapitisha mradi. Kama mwanaharakati, nalidhika kabisa na huduma za Barrick pamoja na viongozi wetu wa serikali," aliongeza Makori.

Miradi hiyo hiyo ya kijamii iliyozinduliwa ni miongoni mwa 101 itakayotekeleza Kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tisa za CSR zilizotolewa na mgodi wa North Mara kutokana na uzalishaji wa mwaka 2023.

Aidha, tayari mgodi huo umetenga kiasi kingine cha shilingi zaidi ya bilioni 4.687 kutokana na uzalishaji wa mwaka 2024 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages