NEWS

Monday, 28 April 2025

Waziri Kikwete aipongeza Barrick kwa matumizi ya teknolojia zenye usalama migodini




Na Mwandishi Wetu, Singida

Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, ameipongeza migodi ya Barrick yenye ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga nchini, kwa kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia Akili Mnemba (AI), vifaa, mitambo ya kisasa ya kidijitali na kulinda usalama na afya za wafanyakazi wake mahali pa kazi.

Waziri Kikwete alisema hayo jana alipotembelea banda la Barrick kwenye maonesho ya OSHA yanayoendelea kwenye viwanja vya Mandewa mjini Singida.

Alisisitiza umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa teknolojia ili kulinda afya za wafanyakazi kwenye sehemu zote za kazi kama vile migodi na viwandani.

“Huko nyuma mlikuwa mnakwenda wenyewe kwenye uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi lakini sasa mnatumia mitambo ili kuweza kufanikisha kazi hii, hongereni sana kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi,” alisema Kikwete alipokuwa kwenye banda la Barrick Bulyanhulu.

Kikwete aliongeza kuwa juhudi za Barrick nchini kwa kushirikiana na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) zimefanikisha kuwepo mazingira rafiki ya ufanyaji kazi ambayo ni chachu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya uchimbaji wa madini.

“Natoa wito kwamba elimu hii ya afya na usalama mahali pa kazi inayoendelea kutolewa kupitia maonesho haya iendelee kutolewa nchi nzima ili kupanua wigo wa uelewa kwa Watanzania, hasa wafanyakazi katika sekta mbalimbali nchini katika kukabiliana na ajali na majanga sehemu za kazi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Aristides Medard, Mtaalam wa Afya na Mazingira kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu, alimweleza Waziri Kikwete na ujumbe wake kuwa kwa kutumia akili mnemba, mgodi huo unaendesha shughuli zake kwa ufanisi na usalama zaidi, hali ambayo inawapa wafanyakazi motisha wa kufanya kazi kutokana na mazingira kuwa rafiki.

Mtaalamu wa Afya na Mazingira kutoka Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Aristides Medard akifafanua jinsi unavyofanya shughuli za uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, vifaa na mitambo ya kisasa na akili mnemba kwa Waziri Ridhiwani Kikwete, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maonesho ya Afya na Usalama Mahali pa kazi yanayoratibiwa na OSHA kwenye viwanja vya Mandewa mjini Singida.
-------------------------------------

Naye Mrakibu Mwandamizi wa Usalama, Meshack Issack, kutoka Mgodi wa North Mara alisema mgodi huo ni kinara wa matumizi ya kidijitali na akili mnemba na mifumo ya kimataifa katika uchimbaji wa madini na afya na usalama nchini.

Mrakibu Mwandamizi wa Usalama wa Mgodi wa North Mara, Meshack Issack (kushoto), akitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu akili mnemba inavyotumika kwenye uchimbaji wa madini kwenye migodi ya Barrick, kwa Waziri Ridhiwani Kikwete, kwenye maonesho ya usalama mahali pa kazi yanayoendelea kwenye viwanja vya Mandewa mjini Singida.
-------------------------------------

Issack aliongeza kuwa mgodi huo na mingine yote ya Barrick inatekeleza program ya “Journey to Zero” ambayo inalenga kuhakikisha kila mfanyakazi anakuwa salama kazini hadi anaporudi nyumbani, na kupaza sauti kunapokuwepo na viashiria vya mazingira hatarishi kwenye maeneo ya kazi.

“Hii programu ya “Journey to Zero” ni DNA ya kampuni, inawahusu pia wakandarasi wa Barrick, wageni wanaotembelea migodi yetu na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akipata maelezo ya moja ya kifaa cha kukaa kinavyofanya kazi kwenye migodi ya Barrick.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages