
Sehemu ya jengo jipya la Kanisa la SDA Mtahuru Mtahuru linaloendelea kujengwa katika mtaa wa Tagota mjini Tarime, Mara.
-----------------------------------
Na Joseph Maunya, Tarime
Shilingi 48,700,550 zimepatikana katika harambee ya kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa jengo jipya la Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Mtahuru lililopo Tagota mjini Tarime, Mara.
Harambee hiyo ilifanyika Aprili 26, 2025 katika viwanja vya kanisa hilo, ambapo mgeni rasmi, Joshua Marwa na rafiki zake pekee walifanikisha upatikanaji wa shilingi zaidi ya milioni 45.
Marwa ambaye ni mshiriki na mzee wa Kanisa la SDA Tarime Central, aliwashukuru rafiki zake kwa michango yao huku akiwahimiza waumini kukua katika matoleo.

Mgeni rasmi, Joshua Marwa (katikati mwenye suti ya bluu), katika picha ya pamoja na waimbaji wa Kwaya ya Vijana ya SDA Tarime Central.
-------------------------------------
"Leo upande wa mgeni rasmi zimepatikana shilingi 45,172,000, benki tayari tumeweka milioni 30, zingine ni ahadi na zile zilizotolewa hapa na marafiki nilioambatana nao, niwashukuru wote kwa kuniunga mkono na niwakumbushe pia waumini wote tukue kimatoleo ili kufanya kazi ya Mungu isonge mbele," alisema.
Marwa aliwataja baadhi ya rafiki zake waliomuunga mkono kuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles "K" na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye "Namba Tatu".

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la SDA Mtahuru, Meshack John, aliwashukuru wote walioshiriki katika harambee hiyo - akiahidi kuwa fedha zote zilizopatikana zitatumika kwa kazi iliyokusudiwa.
"Niwashukuru wote tuliotoa na ambao hatukutoa tujiandae wakati mwingine maana kazi ya Mungu ni endelevu, lakini pia niwahakikishie kwamba kile kilichopatikana kitatumika kwa lengo lililokusudiwa kama ambavyo muongozo unaelekeza," alisema Mchungaji Meshack.

Mchungaji wa Kanisa la SDA Mtahuru, Meshack John, akizungumza wakati wa harambee hiyo.
---------------------------------
Awali, akisoma taarifa fupi ya ujenzi huo, Katibu wa Majengo wa Kanisa hilo, Michael Mbamba, alisema lengo la harambee hiyo lilikua kupata shilingi milioni 57 kwa ajili ya kugharimia kufunga lenta na kuanza upauaji wa jengo jipya la kanisa hilo.



UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Elizabeth Msabi arejea kutoka UK, awa mwanamke wa kwanza kutangaza nia ya ubunge Tarime Vijijini kupitia CCM
»Rorya wamshukuru Katibu Mkuu CCM Balozi Dkt Nchimbi kwa kukazia ujenzi wa barabara ya Utegi - Shirati - Kirongwe kwa lami
»MAKALA:Ujio wa CMG Hotels Ltd utakavyochochea ukuaji wa utalii, uchumi Tarime
No comments:
Post a Comment