NEWS

Monday, 28 April 2025

Rorya wamshukuru Katibu Mkuu CCM Balozi Dkt Nchimbi kwa kukazia ujenzi wa barabara ya Utegi - Shirati - Kirongwe kwa lami



Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi (wa tatu kutoka kushoto), akikaribishwa kuhutubia wananchi wa Rorya wiki iliyopita. Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (kushoto), Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi (wa pili kulia) na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege (wa tatu kulia), miongoni mwa viongozi wengine.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Rorya

Wananchi wa jimbo la Rorya wamemshukuru Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi, kwa kukazia ujenzi wa barabara ya Utegi – Shirati – Kirongwe kwa kiwango cha lami.

Balozi Dkt Nchimbi alikazia ujenzi wa barabara hiyo alipohutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Shirati wakati wa ziara yake ya siku tano mkoani Mara iliyotamatika wiki iliyopita.

“Kipekee, kwa niaba wa wananchi wetu wa Rorya, kwa upendo mkubwa tunamshukuru sana Katibu Mkuu wetu wa CCM kwa kukazia ujenzi wa barabara ya Utegi - Shirati kwenda Kirongwe kwa kiwango cha lami.

“Barabara hii kwetu ni muhimu sana kiuchumi, kibiashara na hata ukuaji wa pato la taifa kwa serikali itakapokamilika,” amesema Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Wambura Chege (CCM) katika taarifa yake kwa umma.

Kwa mujibu wa Chege, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umekuwa ukisubiriwa kwa miaka mingi, na kwamba ukitekelezwa utaboresha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jimbo hilo.

Hivi karibuni, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia ilitangaza tenda ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kuanza na awamu ya kwanza ya Utegi - Shirati (kilomita 27).

Hivyo, Chege ametuma shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa kwa wananchi wa Rorya na mkoa wa Mara, kwa kuidhinisha ujenzi wa barabara hiyo.

Mbunge huyo amesema wananchi wa Rorya sasa wana deni kubwa la shukrani kwa Rais Samia na wamedhamiria kulipa wema huo kwa kumpigia kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

“Kwa niaba wa watu wa Rorya, tunamshukuru sana Mhe. Rais wetu, na kwa hili sisi watu wa Rorya na mkoa wa Mara tuna deni kubwa sana kwake, tunasema wema hulipwa kwa wema, na tupo tayari sasa kura za mwaka huu tulipe wema kwa mazuri haya aliyotufanyia kwa historia toka Rorya kuanzishwa.

“Tunasema asante Dkt Samia, asante Dkt Nchimbi. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” Mbunge Chege amesema kwa msisitizo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages