NEWS

Thursday, 1 May 2025

CCM yapaza sauti kulaani shambulio dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki

Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi


Na Mwandishi Wetu


Chama Cha Mapinduzi kimeongeza sauti yake katika kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt Charles Kitima, na watu wasiojulikana Jumatano wiki hii.


Taarifa iliyotolewa jana mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Emmanuel Nchimbi, imesema kitendo hicho ni cha kikatili kisichojali utu kwa kiongozi wa dini ambaye amejitolea kuihudumia jamii kwa upendo na uadilifu.


Taarifa hiyo ilivitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na tukio hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.


"CCM itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini katika kudumisha na kuendeleza misingi ya amani, umoja wa kitaifa, mshikamano, heshima na kuthamini haki za binadamu," taarifa ilieleza.


Taarifa hiyo ya chama tawala inafuatia taarifa nyingine iliyotolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Eusebius Nzigilwa, ambayo pia ilaani vikali kushambuliwa kwa Dkt Kitima huku ikivitaka vyombo vya usalama kuchunguza kwa makini chanzo cha kitendo hicho cha kinyama.


Kwa mujibu wa taarifa ya TEC, Dkt Kitima alishambuliwa akiwa nyumbani kwake eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam saa usiku.


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  Jumanne Muliro, alisema jana kuwa jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja katika kuisaidia uchunguzi wa tukio hilo.

Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages