
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kushoto) akizungumza na Chifu Deusdedit Masanja wa Himaya ya Sizaki wilayani Bunda leo mjini Musoma.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, leo amekutana na Chifu Deusdedit Masanja wa Himaya ya Sizaki wilayani Bunda na kujadili mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo.
Katika mazungumzo hayo, Chifu Masanja aligusia suala la kukamilishwa kwa malipo yaliyosalia ya fidia kwa wananchi wa kata ya Nyatwali wilayani Bunda ambao wamehamishwa kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Eneo la kata ya Nyatwali lilitwaliwa na serikali likiwa ni ushoroba wa wanyamapori katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
Kutokana na hatua hiyo ya serikali, wananchi waliokuwa wakazi wa eneo hilo ilibidi wahamishwe kwenda maeneo mengine na hivyo kulipwa fidia.
Chifu Masanja alimweleza Kanali Mtambi kuwa uhamisho wa wananchi wa Nyatwali ni suala lililoanza zamani (mwaka 1959) yeye akiwa mdogo na sasa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kulitekeleza kwa kasi na ufanisi wa hali juu na hivyo kuwezesha wananchi kulipwa fidia kwa muda mfupi.
Ushauri wa kitaalamu uliotekelezwa na watafiti wa wanyamapori kuwahamisha wananchi katika kata ya Nyatwali ulifanywa mwaka 1959 lakini ulipaji fidia ulichukua muda mrefu hadi Septemba 2024 Rais Samia alipotoa shlingi bilioni 59 za fidia kuwalipa wananchi hao.
Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Mkoa, Chifu Masanja amesema kutokana na kazi nyingi alizozifanya Rais Samia katika maeneo mbalimbali nchini, hakuna kitu kitakachomzuia kupata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba.
Amesema uhamasishaji wa Rais Samia wa kutumia nishati safi ya kupikia umeokoa mazingira katika wilaya ya Bunda, ambapo sasa wananchi wengi wameachana na matumizi ya kuni ili kurejesha uoto wa asili.
Chifu Masanja ameeleza kufurahishwa kwake na uteuzi wa Rais wa viongozi waadilifu wanaoongoza mkoa wa Mara ambao amesema ni wachapakazi, wenyenyekevu na wasikivu kwa shida za wananchi.
No comments:
Post a Comment