NEWS

Wednesday, 4 June 2025

Ryakitimbo aichambua Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030



Moses Wambura Ryakitimbo

Na Mwandishi Wetu

Mei 30, 2025, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizindua Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2025-2030, huku ikitarajiwa kutoa majibu ya changamoto na kubadili maisha ya wananchi, ikiwemo mikakati ya kuongeza ajira.

Ilani hiyo iliyozinduliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho tawala.

Ilani hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa kasi ya maendeleo ya nchi kutokana na vipaumbele vinavyolenga kuimarisha maendeleo ya jamii na kiuchumi.

Kada wa CCM kutoka wilaya ya Bunda mkoani Mara, Moses Wambura Ryakitimbo, ambaye ni msomi mbobevu wa masuala ya biashara, uchumi na uwekezaji, amesifu ilani hiyo akisema imeangazia miradi mikubwa ya kimkakati, ukuzaji wa viwanda, demokrasia, elimu, kilimo na mifugo ili kufanikisha kujenga uchumi wa wananchi na kuwawezesha kuzalisha bidhaa kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

“Ilani imeelekeza namna wananchi wanavyoweza kutumia rasilimali kama vile madini, ardhi, utalii, kilimo, mifugo na misitu ili kujiletea maendeleo yao,” Ryakitimbo anasema.

Anaongeza kuwa ilani hiyo imelenga kukuza uchumi wa kisasa kwa kutumia teknolojia za kisasa, jambo ambalo linaendana na mahitaji ya dunia ya leo.

Miongoni mwa ahadi zilizomo kwenye ilani hiyo ni kuzalishwa kwa ajira milioni nane kwa vijana katika kipindi cha miaka mitano ijayo, zikiwemo rasmi na zisizo rasmi.

Kwa sasa, tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa kwani wahitimu wengi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati wanakaa mitaani bila ya ajira.

Ilani hiyo imeilekeza serikali kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kimkakati kwa kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji kampuni za vijana za vyama vya ushirika (Saccos) vyenye kujiendesha kibiashara katika halmashauri zote nchini.

Lengo ni kuwezesha kampuni hizo kupata mikopo na nyenzo za kuwawezesha vijana kujiajiri na kutoa ajira kwa wenzao, ikiwemo na vituo vya mafunzo ya ufundi stadi.

Ilani ya uchaguzi imeweka dhamira ya kukuza sekta ya viwanda kwa wastani wa asilimia tisa kila mwaka. Hii itasaidia kukuza uchumi wa taifa ili kujitosheleza na hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuchangia ongezeko la ajira na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Ryakitimbo anasema wazo la kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kwenye kila wilaya na kutunga sera na sheria itakayozuia kusafirisha nje ya nchi bidhaa zitokanazo na rasilimali za asili bila kuongezewa thamani itanufaisha wakulima na kufufua viwanda katika mkoa wa Mara.

“Shughuli za uwekezaji katika mkoa wa Mara zilitatizika baada ya viwanda kufungwa hali iliyotishia maelfu ya ajira na serikali kupoteza mapato,” anasema na kuendelea:

“Viwanda kama vya nguo, maziwa na kuchakata samaki kama vile Mara Milk Ltd, Musoma Textile Mills Ltd (Mutex), Prime Catch Exporters na vinginevyo vilifungwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile ushindani wa nguo zinazoingia nchini bila kulipiwa ushuru, umeme, uwepo wa tozo nyingi na gharama kubwa za uendeshaji.”

Hata hivyo, serikali imeanza kutatua changamoto za ukosefu wa malighafi za pamba na samaki kwa kuweka mkakati maalum wa kuzuia uvuvi haramu na kusimamia kilimo cha pamba.

Pia, CCM kupitia ilani yake mpya itaweka mazingira maalum ya kuvutia ujenzi wa viwanda vidogo vijijini kwa lengo la kufanya ongezeko la awali la thamani katika sekta za kimkakati, zikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

Lengo la uwekezaji huo ni kuongeza fursa za ajira na kupunguza upotevu wa mazao, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya masoko ikijumuisha vituo vya ukusanyaji na uongezaji thamani.

“Mkoa wa Mara unaolima kwa wingi mazao ya mahindi, viazi, mtama, ulezi, pamba, mihogo na mazao mengineyo, una nafasi kubwa ya kunufaika na ilani hii, kwani viwanda vidogo na vya kati vinaweza kujengwa vingi na hivyo kutoa ajira,” Ryakitimbo anasema.

Kwa mujibu wa mwanachama huyo wa CCM, viwanda vingi vya biskuti vilivyopo Dar es Salaam na Nairobi, Kenya vinatumia malighafi ya viazi vitamu kutoka mkoa wa Mara, ambao ni wazalishaji wakubwa.

“Vilevile, wana-Mara wazalishe zaidi zao la muhogo ili waweze kulikamata soko la China kwa kulitoa katika zao la chakula na kuwa zao la kibiashara kuwezesha pato la mkulima kukua,” anasema.

Anaendelea “China ina uhitaji mkubwa wa unga wa muhogo ambao ni malighafi katika viwanda vya bia, pipi, karatasi, vitafunwa, nguo, rangi na madawa. Hivyo, ilani ya uchaguzi kuja na wazo la kujenga viwanda vya kuongeza thamani inakwenda kujibu kila kitu.”

Katika miaka mitano, Serikali ya CCM inalenga kuanzisha na kutekeleza Gridi ya Taifa ya Maji itakayotumia vyanzo vikubwa vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na umwagiliaji.

Mkoa wa Mara utakuwa mnufaika mkubwa wa gridi hiyo kutokana na kuwa karibu na chanzo kikuu cha maji cha Ziwa Victoria. Tatizo la upatikanaji wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi, kwani kwa sasa huduma ya maji haijakidhi mahitaji ya wananchi, hususan maeneo ya vijijini.

Gridi hiyo itakuja sambamba na bomba maalum la maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji mashambani na mifugo.

“Watu wengi waliushangaa mkoa wetu kufanya shughuli za kilimo kwa kutegemea mvua za msimu wakati tuna chanzo cha maji ya umwagiliaji cha muda wote,” Rayakitimbo anasema.

Kutokana na wingi wa mifugo iliyopo mkoa wa Mara, ilani imeweka lengo na kupima na kutenga hekta milioni tatu hadi kufikia mwaka 2030 kwa ajili ya kupunguza, ama kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Wafugaji watawezeshwa kufanya ufugaji wa kisasa na wa kibiashara kwa kuwa na mifugo michache yenye tija na mafunzo ya kuongeza thamani ikiwemo unenepeshaji.

“Wingi huu wa mifugo, mkoa wetu utaweza kujenga viwanda vingi vya maziwa na nyama kwa soko la ndani na nje ya nchi, viwanda vya viatu na mabegi ya Ngozi,” anasema.

Ilani ya Uchaguzi kuja na wazo la kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo kila wilaya tutatengeneza ajira, kwani ajira zitaongezeka kutoka mashambani kwenda kwenye viwanda vidogo na sokoni.

“Kuuza mazao ghafi tunauza hadi ajira za wananchi wetu, kwani huko nje wanaajiriwa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hizo hizo. Vilevile, kiuchumi nchi inapoagiza bidhaa kutoka nje maana yake mnautoa umasikini nje na kuuleta ndani ya nchi yenu na kutengeneza ajira nje, na mnapouza nje bidhaa zilizoongezewa thamani mnaupeleka umasikini nje na kutengeneza ajira ndani ya nchi,” Ryakitimbo anaeleza.

“Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030 imelenga kuboresha bandari mbalimbali nchini, ikiwemo ya Musoma, mkoani Mara. Bandari hii tunapaswa kuendelea kuitumia katika kukuza uchumi wa mkoa wetu,” anasema.

Anaongeza kuwa uboreshaji wa bandari hiyo utaleta ajira mpya, ukuaji wa biashara na ongezeko la fursa za masoko zitakazotokana na mwingiliano wa wafanyabiashara na wananchi na nchi jirani na mkoa wa Mara.

“Eneo la bandari yetu lina kina kirefu kinachofaa kuwa bandari kubwa Afrika Mashariki, ambayo ikiunganishwa na reli kutoka Mwanza na ile ya kutoka Arusha itaufungua uchumi wa mkoa wa Mara, sambamba na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma unaoendelea na ujenzi mpya wa Uwanja wa Ndege Serengeti uliopo katika ilani hiyo mpya ya CCM.

“Mkoa wa Mara una madini mengi ya aina mbalimbali - ambayo bado hayajanufaisha wananchi wetu kikamilifu. Kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030 kwa kutambua madini yanaweza kuchangia fursa za ajira, pato na uchumi wetu, wameweka lengo la kuona sekta ya madini inakua kwa wastani wa angalau asilimia saba kwa mwaka.

“Ili kufikia azma hiyo wanatarajia kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo wa madini, kuwapatia leseni na kuwaendeleza. Vilevile, kufanya utafiti zaidi wa maeneo yenye madini na kuongeza eneo lililopimwa na kufanyiwa utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030,” Ryakitimbo anasema.

Kwenye sekta ya utalii lengo la ilani ya uchaguzi ni kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa kutoka asilimia 17 mwaka 2025 hadi asilimia 20 mwaka 2030, kwa kuanzisha kampeni maalum ya kufikisha idadi ya watalii milioni nane kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.

“Kutokana na mkoa wetu wa Mara kuwa na Hifadhi ya Taifa Serengeti na Ziwa Victoria, tuna nafasi kubwa ya kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni na hivyo kuweza kunufaika na ajira milioni tatu zinazotarajiwa kutengenezwa kupitia ilani hii, ikiwamo waongoza utalii, usimamizi wa hoteli, huduma kwa wateja na zinginezo.

“Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Serengeti utaleta watalii wengi mkoa wa Mara kuliko watakaokuwa wanashukia Kilimanjaro na Arusha.

“Tunaamini wananchi watatumia fursa zilizomo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030 ili kujiletea maendeleo binafsi na jamii wanazotoka kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia rasilimali zilizopo, kwani ilani hii inatekelezeka - na kihistoria hakuna sekta ambayo iliwekewa malengo katika ilani na hayakufikiwa,” Ryakitimbo anahitimisha.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages