
Meneja Msaidizi wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Nasieku Kisambu (katikati), akizungumza katika moja ya mikutano ya kusikiliza malalamiko na maoni ya wananchi katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umeendesha kliniki ya kusikiliza malalamiko na maoni mbalimbali ya wananchi katika vijiji 11 vinavyouzunguka wilayani Tarime, Mara.
Vijiji vilivyotembelewa ni Mjini Kati, Nyangoto, Kewanja, Matongo, Nyabichune, Kerende, Nyakunguru, Komarera, Genkuru, Msege na Nyamwaga.
Madhumuni ya ziara ya hiyo iliyochukua takriban wiki moja ni kuupa mgodi wa North Mara nafasi ya kujibu hoja na malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa vijiji hivyo.
Lengo jingine ni kuelimisha jamii kuhusu uwepo wa chombo cha mgodi huo cha kushughulikia malalamiko, kuelezea habari na kufafanua dhana potofu zilizopo katika jamii kuhusu mgodi huo.
Mafanikio ya ziara hiyo ni pamoja na kueleweka kwa mfumo wa Mgodi wa Dhhabu wa North Mara wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi miongoni mwa jamii inayouzunguka.
Mgodi huo kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kujibu hoja na malalamiko yaliyotolewa na wananchi, na hivyo kujenga hali ya mshikamano na kuaminiana baina ya pande hizo mbili.
Katika miaka ya karibuni, mgodi wa North Mara umekuwa chachu ya maendeleo kwa vijiji vinavyouzunguka kwa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility - CSR).
Hata vijiji ambavyo vipo nje ya maeneo ya mgodi huo hivi sasa vinanufaika na ‘keki’ ya CSR kutoka katika mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Sekta za kijamii zilizonufaika zaidi kutokana na fedha za CSR na mrabaha kutoka Barrick North Mara ni elimu, afya, maji, barabara na uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi kwa wananchi ili kuwawezesha kuinua hali zao za maisha.
Mgodi wa Barrick North Mara pia unachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kutoka sekta ya madini.
No comments:
Post a Comment