NEWS

Tuesday, 3 June 2025

Uwanja wa Ndege Serengeti rasmi kwenye Ilani ya CCM 2025-2023



Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan, Makamu wake, Stephen Wasira (wa nne kulia), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwingi (wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakionesha vitabu vya Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025-2030 mara baada ya kuizindua wiki iliyopita jijini Dodoma.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti mkoani Mara ambao kwa miaka 20 umekuwa ukisuasua sasa umepata msukumo mpya baada ya utekelezaji wake kuingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025-2030.

Ilani hiyo mpya ya CCM ilizinduliwa rasmi Mei 30, 2025 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho tawala.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo mpya ya CCM, uwanja huo ni moja ya miradi kadhaa ya viwanja vya ndege nchini iliyopangwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.

Lengo kubwa la ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti ni kuufanya mji wa Mugumu ambao ni makao makuu ya wilaya ya Serengeti kuwa kitovu cha utalii katika Hifadhi kongwe ya Taifa ya Serengeti ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii duniani.

Ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka nje kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu, ambao mamlaka zimekuwa zikijadiliana kubadili jina lake liwe Serengeti.

Pia, kujengwa kwa uwanja huo kutasaidia kupunguza idadi ya ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kusaidia kufungua fursa za kiuchumi wilayani Serengeti na taifa kwa ujumla.

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya usafiri wa anga nchini imeshika kasi kufuatia ujenzi wa barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege na kuboreshwa kwa usafiri wa majini katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Uimarishwaji wa viwanja vya ndege umewavuta watalii wengi kutembelea maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuliwezesha taifa kukusanya fedha nyingi za kigeni.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030 pia imejumuisha ujenzi wa barabara ya lami ya Tarime hadi Mugumu, ikiwa ni jitihada za kuunganisha wilaya mbili za Tarime na Serengeti kwa barabara ya lami.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages