
Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wakishirikiana na wananchi kupanda miti ya asili kandokando ya mto Tighite wilayani Tarime, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5, 2025.
-----------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara leo umeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupandaji miti ya asili ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda kingo za mto Tighite uliopo jirani na mgodi huo wilayani Tarime, Mara.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu kwa upande wa Tanzania inasema "Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo – Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki".
Viongozi wa mgodi wa North Mara wameshirikiana na Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, viongozi wa vijiji na kata jirani kupanda miti ya asili kandokando ya mto huo katika kijiji cha Matongo.

Upandaji wa miti ukiendelea.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko, amesema hiyo ni hatua ya awali ya utekelezaji wa programu ya kupamda miti 50,000 kwenye kingo za mto huo katika vijiji 13 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
“Mbali na kupanda miti ya asili kwenye kingo za mto huu, tutapanda miti ya mbao nje ya mita sitini kutoka mtoni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kwa jamii,” amesema Lyambiko.


Meneja Mkuu wa mgodi, Apolinary Lyambiko, akipanda mti wa asili kandokando ya mto Tighite.
---------------------------------------
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, Mwita Seri, amesema miti hiyo pia itasaidia kurejesha uoto wa asili na kuimarisha usalama wa maji ya mto huo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Mkazi wa kijiji cha Msege, Sarah Lucas, ameushukuru mgodi huo kwa kuendelea kushirikiana na jamii katika kutunza mazingira, akisema jitihada kama hizo zinasaidia kuleta maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya wananchi.
“Miti hii tunayopanda ikikua itasaidia pia kuleta mvua na kuzuia upepo mkali katika maeneo yetu,” Sarah amesema.

Sarah Lucas akizungumza eneo la tukio.
--------------------------------------
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba na Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Faustine Chacha, wameahidi kusimamia utunzaji wa miti hiyo ili kulinda bioanuwai ya mto huo.
Naye Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, amesema mgodi huo unashirikiana vizuri na jamii inayouzunguka, ikiwemo Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini iliyobuni wazo la kupanda miti hiyo.

Meneja Mahusiano, Francis Uhadi (kulia), akizungumza kwenye eneo la tukio. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi, Apolinary Lyambiko na katikati ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, Mwita Seri.
-------------------------------------------
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka, ikiwa ni jukwaa la kimataifa la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzanzia kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Picha ya pamoja
No comments:
Post a Comment