NEWS

Sunday 3 May 2020

Muhongo aongeza ufanisi kwenye kilimo Musoma Vijijini

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea kutekeleza programu ya uboreshaji kilimo jimboni kwa kuhamasisha uanzishaji vikundi vya wakulima na kuvigawia plau na mbegu bora za mazao mbalimbali.

Msaidizi wa mbunge huyo, Verediana Mgoma, ameiambia Mara Online News leo Jumapili Mei 3, 2020 kwamba tayari vijiji 86 vimeanzisha vikundi hivyo na vimeanza kugawiwa plau zinazotolewa na Profesa Muhongo.
Wakulima wakiwa kazini Musoma vijijini

Mgoma amesema tayari plau 45 zimeshagawiwa kwa vindundi 45 vya wakulima na kwamba mbunge huyo amejipanga kugawa nyingine 40 wakati wa Sikukuu ya Eid El Fitr baadaye mwezi huu.

Pia Mbunge Muhongo amekuwa akigawa kwa vikundi vya wakulima mbegu bora za mazao ya alizeti, mihogo, mtama na ufuta tangu mwaka 2016.

Profesa Muhongo
Naye Profesa Muhongo amesema ugawaji wa plau na mbegu bora ni mwendelezo wa programu ya kuboresha kilimo jimboni humo kwa kuwezesha wakulima kuondokana na jembe la mkono, hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na kujitosheleza kwa chakula.

Wanachama wa vikundi vya wakulima katika jimbo la Musoma Vijijini wamemshukuru mbunge wao huyo kwa hatua hizo za kuwaongezea ufanisi kwenye kilimo.

(Habari na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages