WANAFUNZI wa kidato cha sita waliokuwa likizo mkoani Simiyu,
wamepokea kwa furaha tamko la serikali la kufungua shule kuanzia Juni 1, 2020,
huku wakisema wamejipanga vizuri kuelekea mtihani wa taifa wa kidato hicho.
Wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti mjini
Bariadi, Simiyu Mei 27, 2020, wamesema wameweza kutumia likizo ya dharura
iliyoitishwa na serikali kupisha mapambano dhidi ya virusi vya corona,
kujiandaa kwa ajili ya mitihani ya mwisho.
"Ilikuwa nimalize mtihani wangu wa NECTA Mei 22, mwaka
huu maana nachukua PCB, lakini virusi vya corona vikaniharibia," amesema Thomas
Mwambilija, mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana
Ihungo iliyopo mkoani Kagera.
Mwambilija ameongeza "Nilikuwa nimejiandaa vya kutosha,
corona ilivyoingia ikaharibu kila kitu, lakini naishukuru serikali kwani
likizo ya dharura imenisaidia kujiandaa vya kutosha, nimejisomea na nipo tayari
kwa mtihani."
Hilda Revocatus, mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule
ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Ihunyo iliyopo mkoani Mara, amesema janga
la corona lilitaka kuua ndoto zake, lakini amefurahi shule kufunguliwa na
kwamba amejipanga vyema kumalizia vipindi vya masomo vilivyobaki.
Wanafunzi hao pia wameishukuru serikali kipitia Wizara ya
Elimu kwa kuunda mpango maalumu uliowawezesha kusoma kwa njia ya mtandao wakiwa
likizo nyumbani, ambao umewasaidia kufanya marudio ya masomo yote.
Katika hatua nyingine, wanafunzi hao wamempongeza Rais Dkt
John Magufuli kwa hotuba zake mbalimbali ambazo zimesaidia wananchi
kupunguza hofu ya corona nchini.
(Imeandikwa
na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment