Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imebaini ufisadi wa Zaidi Ya shilingi
Bilioni 3 katika malipo ya fidia kwa
wananchi wa kijiji cha Matongo kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, yaliyofanywa
na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima(kulia) akitoa maagizo mbalimbali kuhusu ufisadi ambao umefanywa Nyamongo |
Taarifa iliyotolewa na
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Alex Kuhanda kwa waandishi wa habari mjini
Tarime leo Juni 10, 2020, imesema Sh 2,127,236,784 ni malipo hewa ya fidia ya
nyumba za wananchi hao na Sh 1,143,796,786.28 ni malipo hewa ya posho ya
usumbufu wa kuhama kutoka kwenye nyumba hizo.
Kuhanda amesema uchunguzi
wa ofisi yake umebaini kwamba malipo stahiki ya fidia kwa wananchi hao ni Sh
226,858,656.52 na siyo Sh 3,482,988,360 zilizolipwa kama fidia ya nyumba hewa 72 za
wananchi hao.
Mkuu wa TAKUKURU Mara Alex Kuhanda akieleza udanganyifu katika zoezi la malipo ya fidia |
RPC William Mkonda(kushoto) na RPC Daniel Shilla (kulia) wakiteta baada ya kupokea maagizo ya RC Malima |
“Tuna watendaji wa
Serikali, wote wakamatwe na wafunguliwe mashitaka kwa kujaribu kuibia Serikali.
Viongozi wa vijiji, viongozi wa vitongoji wote waliohusika wakamatwe,” ameagiza
Malima katika kikao hicho.
Alisema uchunguzi zaidi
juu ya ufisadi unaohusisha Sh zaidi ya bilioni tano unaendelea na ikibainika
hata wafanyakazi wa mgodi wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick
wamehusika watatiwa mbaroni.
“Pia kwenye tasisi za kifedha
[benki] uchunguzi ukibaini wamehusika tunawachukua,” ameongeza Malima.
Hata hivyo, mkuu huyo wa
mkoa amesema baadhi ya watuhumiwa wa
ufisadi huo wameanza kujisalimisha, huku akiwataka wananchi wote wenye uhakika
kuwa maombi ya fidia zao ni halali kuendelea kuchukua noti zao.
(Habari, picha na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment