NEWS

Friday 7 August 2020

Wananchi wachangamkia upimaji masikio Nanenane Simiyu

Sista Dkt Sophia Mbihije (kulia), akielimisha wananchi wakiwamo wanafunzi kwenye maonesho ya Nanenane, Nyakabindi.
 

WANANCHI zaidi ya 100 wamefikiwa na huduma ya uchunguzi wa masikio inayotolewa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo cha mkoani Tabora ambacho ni tawi la Chuo Kikuu cha Tanzania cha Matakatifu Augustino (SAUT), kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi, wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

 

Hayo yamesemwa na Mhadhiri wa chuo hicho, Sister Dkt Sophia Mbihije na kuongeza kuwa chuo chao kinatoa shahada mbalimbali ikiwemo elimu ya uchunguzi wa masikio, mahitaji maalumu, sanaa na utawala katika biashara na kwamba wameshiriki maonesho hayo kuwashirikisha wananchi umuhimu wa shahada hizo muhimu katika jamii.

 

Sista Dkt Mbihije amesema chuo hicho kinafundisha uchunguzi wa masikio ili kujua chanzo cha matatizo hayo na namna ya kuyatatua na kwamba wahitimu wanaotoka hapo wanaweza kuajiriwa, au kujiajiri na kusaidia wahitaji katika jamii.

 

Ameongeza kuwa wanawatayarisha walimu kwa ajili ya kufundisha shule za sekondari ili kukidhi mahitaji ya watoto wenye mahitaji maalumu, hususan viziwi na wasioona na kwamba ili mwalimu aweze kumhudumia mwanafunzi lazima ajue lugha ya alama na mwanafunzi akiishajua lugha hiyo humsaidia na yeye baadaye kuwa mkarimani katika ofisi mbalimbali za umma na binafsi.

 

Sista Dkt Mbihije amefafanua kuwa shahada wanazotoa ni pamoja na kutayarisha walimu kuwa na uwezo wa kufundisha watu wenye mahitaji maalumu wakiwamo viziwi na wasioona ili baadaye nao wawe wataalamu wa kukarimani.

 

Amesema ni matumaini yao kwamba kupitia maonesho hayo, wananchi wataitikia kufika kwenye banda lao kupata elimu ya namna ya kujiunga na chuo hicho sambamba na kupata huduma ya kupima masikio bila malipo.

Lukonge John (aliyesimama) akitoa huduma ya upimaji wa sikio kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda lao kwenye maonesho ya Nanenane, Nyakabindi.

Naye Lukonge John kutoka chuo hicho amesema tangu wafike kwenye maonesho hayo wameweza kuwahudumia watu mbalimbali, wengi wao wakitoka Kanda ya Ziwa. Amtoa mwito kwa wazazi na walezi kuchangamkia fursa hiyo ya kupima masikio bure, lakini pia kujiunga na chuo chao.

 

Nao baadhi ya wananchi waliotembelea banda la chuo hicho, hususan wenye matatizo ya masikio wamesema huduma zinazotolewa ni za uhakika na hazina gharama yoyote.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages