NEWS

Thursday 6 August 2020

Waziri Hasunga aongeza siku mbili maonesho ya Nanenane

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza katika maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga.
  

KUTOKANA na uhitaji mkubwa na baadhi ya wadau kuchelewa kuanza maonesho ya Nanenane mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameongeza siku mbili za maonesho hayo kwa kanda zote nchini ambapo badala ya Agosti 8, sasa yatahitimishwa Agosti 10.

 

Waziri Hasunga ametoa tamko hilo Agosti 4, 2020 alipozungumza na wadau kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu ambako maonesho ya Nanenane yanafanyika kitaifa.

 

Amesema ongezeko la siku mbili litakidhi mahitaji ya wakulima ya kujifunza mbinu bora za kilimo, lakini pia wananchi ambao hawakupata fursa awali watatumia siku hizo za nyongeza kujionea mbinu na teknolojia bora za kilimo, mifugo na uvuvi.

 

Kwa mujibu wa Waziri Hasunga, malengo makuu ya maonesho hayo ni pamoja na kuwaunganisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika katika kusherehekea na kuonesha teknolojia na zana bora za kilimo, Mifugo na Uvuvi.

 

Mbali ya kuwakutanisha wakulima, wavuvi na wafugaji, amesema maonesho ya Nanenane ni fursa ya kuwakutanisha watoa huduma za fedha, bima, mawasiliano, taasisi za umma na binafsi.

 

Kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020”.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (kulia), akiangalia bidhaa kwenye banda katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi, wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
 

Kupitia kaulimbiu hiyo, Waziri Hasunga amewaomba wananchi wakiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na kuchagua viongozi bora kwa kuzingatia maemndeleo makubwa ya sekta mbalimbali nchini zikiwemo za kilimo, mifugo na uvuvi yaliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

 

Akizungumza baada ya tamko la Waziri Hasunga, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amewataka wadau kuzitumia vizuri siku zilizoongezwa za maonesho ya Nanenane kwa kujitokeza kwa wingi kujifunza mambo ambayo wangeyakosa endapo muda usingeongezwa.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Nanenane, Luteni Kanali Peter Lushika kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), amesema wadau wamepokea kwa furaha tamko hilo la Waziri Hasunga kwani litawapa fursa ya kujifunza zaidi teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

 

Luteni Kanali Lushika ametumia nafasi hiyo pia kutoa mwito kwa wananchi kutembelea banda la JKT ili kujifunza teknolojia nyingi, hatua itakayowawezesha kubadilisha mfumo wa utendaji kazi zao na kuwasaidia kuongeza thamani ya mazao na bidhaa wanazozalisha.

 

Naye aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, amesema maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yana maboresho makubwa ya mazao na teknolojia nyingi na kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu itakayowawezesha kuboresha na kuongeza tija katika shuguli za kilimo, mifugo, uvuvi, miongoni mwa nyingine.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages