NEWS

Sunday 9 August 2020

Waziri Mpango aipongeza TRA, aitaka iongeze makusanyo

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango (katikati), akitoa melekezo kwenye banda la TRA katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.
 

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri ya kukusanya mapato ya serikali, huku akiitaka kuongeza makusanyo ya kodi kutoka wastani wa Sh trilioni 1.5 za sasa hadi trilioni mbili kwa mwezi.

 

Waziri Mpango ametoa pongezi na maagizo hayo wakati alipotembelea banda la TRA kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.

 

“Nawapongeza lakini bado ningependa serikali ikusanye trilioni mbili kwa mwezi, uwezo wa kukusanya trilioni mbili upo, na niishauri TRA kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mapato yanaongezeka kufikia kiwango hicho,” alisema Waziri Mpango.

 

Ameongeza kuwa lazima nchi yetu ijitegemee kwani ina uwezo wa kuondoka katika uchumi wa kati na kufikia uchumi wa juu endapo dosari ndogondogo zilizopo katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato zitaondolewa.

 

Hata hivyo, waziri huyo amesema ukusanyaji mdogo wa kodi unatokana na kuwepo kwa watu wanaokwepa kodi, hivyo kuitaka TRA kudhibiti upotevu wa vyanzo vya mapato na kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi kwa kuongeza idadi ya walipakodi kwani pamoja na Tanzania kuwa na watu takriban milioni 60, ni watu takriban milioni mbili wanaolipa kodi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango (kulia), akisaini kwenye kitabu cha wageni kwenye banda la TRA katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.
 

Kuhusu kodi ya majengo, Waziri Mpango ameiagiza TRA kukusanya kwa ufanisi akisema  majengo ni mengi ila kodi inayokusanywa ni ndogo, hivyo kuna haja ya kuweka mkakati wa  kuhakikisha majengo yote yanayostahili yanalipiwa kodi.

 

Ameongeza kuwa mapato yataongezeka endapo watumishi wasio waadilifu hususan katika idara ya forodha watashughulikiwa na ikibidi kuwafukuza kazi ili wabakie wachache waadilifu kwani ni eneo ambao linalalamikiwa sana.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mpango amempongeza kwa kipekee Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, kwa jitihada anazofanya katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya kodi na kushauri nguvu zaidi katika kuelimisha wananchi namna nzuri ya kulipa kodi na kuwasilisha ritani za kodi kwa wakati.

 

Amesema kutokana na kiwango cha elimu kwa wananchi kuwa kidogo, TRA haina budi kuwa rafiki, kuwasikiliza na kuwaelimisha walipakodi namna nzuri ya kulipa kodi na kuwa sehemu ya kuwasaidia kukuza biashara zao badala ya kufunga biashara ili kupata mapato zaidi.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages