NEWS

Monday 28 September 2020

Kishindo cha Chege Rorya, aahidi daraja, zahanati Kerogo

Mgombe ubunge katika jimbo la Rorya kwa tiketi ya CCM, Jafari Chege (kulia) akiomba kura kwa mamia ya wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza kumsikiliza katika mkutano wake wa kampeni katani Kerogo, leo Septemba 28, 2020. (Picha na Peter Hezron)

MGOMBEA ubunge jimbo la Rorya kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jafari Chege ameahidi kwamba akichaguliwa atahakikisha wakazi wa kata ya Kerogo wanajengewa zahanati na daraja la kisasa mto Mori.

 

“Ninawaahidi kwa moyo wa dhati, nipeni kura nyingi za ubunge na mpeni Rais John Magufuli kura nyingi anipe nguvu ya kupata fedha serikalini kwa ajili ya kuwajengea daraja kubwa la mto Mori,” Chege ameuambia umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza kumsikiliza katani Kerogo leo Septemba 28, 2020.

Mamia ya wananchi wakimsikiliza na kumshangilia mgombea ubunge jimbo la Rorya kwa tiketi ya CCM, Jafari Chege (hayupo pichani) katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katani Kerogo leo Septemba 28, 2020. (Picha na Peter Hezron)

 

Amesema ujenzi wa daraja hilo utatekelezwa sambamba na uchongaji wa barabara zitakazopitika kirahisi muda wote na kuunganisha kata hiyo na upande wa pili, hatua itakayowaondolea wananchi adha ya kuzunguka umbali mrefu kupitia Ingri wakati wa kusafiri kwenda wilaya jirani ya Musoma.

Baadhi yua wananchi wakicheza na kumshangilia mgombea ubunge jimbo la Rorya kwa tiketi ya CCM, Jafari Chege (hayupo pichani) katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katani Kerogo, leo Septemba 28, 2020. (Picha na Peter Zabron)

 

Kuhusu zahanati, mgombea huyo kijana ameahidi kwamba akipata ridhaa ya wananchi ya kuwa mbunge wa Rorya atahakikisha ujenzi wa mradi huo wa afya unaanza Januari na kukamilika Juni 2021.

 

“Naahidi kutoka moyoni, endapo mtanichagua, kuanzia Januari nitaleta mabati 100 mimi mwenyewe kwa ajili ya kuezeka zahanati, kisha nitaanza kuchangisha fedha za kugharimia ukamilishaji wake ili kabla ya Juni [mwakani] iwe imekamilika,” amesisitiza Chege.

 

Ameongeza kwamba kwa kuwa Ilani ya CCM imeelekeza kila kata iwe na kituo cha afya, atahakikisha anaiombea zahanati hiyo ipandishwe hadhi kuwa kituo cha afya kabla hajamaliza miaka mitano ya ubunge wake.

Mgombea ubunge jimbo la Rorya kwa tiketi ya CCM, Jafari Chege (katikati) akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa wazee maarufu ili aweze 'kuwika' kama jogoo huyo bungeni. Tukio hilo limefanyika katani Kerogo leo Septemba 28, 2020 alipokwenda kuomba kura. (Picha na Peter Hezron)


“Nitaboresdha pia sekta ya kilimo kwa kuhakikisha tunaanzisha zao la biashara, lakini nitaanza na barabara ili mkilima mpate daraja na barabara kwa ajili ya kusafirisha mazao, hiyo nimesema nitaisimamia kwa dhati, lazima niwasimamie kwa yale yote mnayoyahitaji,” amesema Chege.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages