NEWS

Monday 21 September 2020

Waganga tiba asili Simiyu waahidi ushirikiano serikalini

Waganga wa tiba asili na mbadala wakifuatilia mtoa mada kwenye uzinduzi wa kampeni ya kimkoa ya kuhamasisha wananchi kuchangia damu uliofanyika wilayani Itilima jana.



WAGANGA wa tiba asili na mbadala mkoani Simiyu wameahidi kupitia umoja wao kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu ili kuokoa maisha ya wahitaji wa huduma hiyo.

 

Pia wameahidi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujisajili kwa ajili ya kutambulika kisheria hatua itakayowahalalisha kufanya kazi zao na kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi.


Wamesema hayo wilayani Itilima jana, kupitia taarifa yao iliyosomwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt Khamis Kulemba katika uzinduzi wa kampeni ya kimkoa ya kuhamasisha wananchi kuchangia damu salama na kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi (kulia) akichangia damu wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika kimkoa wilayani humo, jana.

 

Kwa mujibu wa Dkt Kulemba, mkoa wa Simiyu una waganga 4,353 wa tiba asili na mbadala, kati ya hao, wenye leseni ni 29 na waliopeleka maombi kwenye Baraza la Tiba Asili kwa ajili ya kupata leseni ni 398.

 

Dkt Kulemba amEsema kwamba Agosti 19 na 20, 2020 idara ya afya mkoa humo ilifanya kikao na waganga hao wakakubaliana kuhakikisha wanatoa rufaa kwa wateja wao wenye dalili za magonjwa sugu mapema, kujitokeza kuchangia damu na kuhamasisha jamii inafanya hivyo ili kuokoa maisha.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi (kulia) mara baada ya kuchangia damu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kimkoa ya kuhamasisha wananchi kuchangia damu uliofanyika wilayani humo, jana.

 

Awali, akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Elizabeth Gumbo, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt Anold Musiba amesema kundi hilo (waganga wa tiba asili na mbadala) limejitokeza kwa wingi kuchangia damu.

 

“Waganga wa tiba asili na mbadala wamekuwa wakitoa tiba mbadala katika jamii kwa ufasaha, kushiriki kwa ukaribu shughuli za kijamii na za kiserikali wilayani kwetu (Itilima) na idadi kubwa ya waganga wametambulika,” amesema Dkt Musiba.

 

Aidha, amesema halmashauri hiyo inaendelea kufanya ufuatiliaji na utambuzi wa waganga wa tiba asili na mbadala kwa ajili ya kuwapatia leseni kwa mujibu wa Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Tiba Asili na Mbadala Na. 23 ya Mwaka 2002 na Kifungu cha 3 cha Kanuni za Usajili.

 

Dkt Musiba ameongeza kuwa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Itilima inaendelea kuhamasisha wataalamu wa tiba asili na mbadala kujiunga na Baraza la Tiba Asili na Mbadala ili waweze kupatiwa leseni za taaluma za kazi zao.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliyealikwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huu, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi ameutaka uongozi wa sekta ya afya mkoani humo kuwasaidia waganga wa tiba hizo kusajiliwa na idara ya maliasili kutoa elimu ya usajili wa nyara za serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi (kushoto) akikabidhi vyeti kwa baadhi ya waganga wa tiba asili na mbadala waliosajiliwa. Shughuli hiyo ilifanyika wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kimkoa ya kuhamasisha wananchi kuchangia damu uliohudhuriwa na waganga hao wilayani humo, jana.

 

Meneja Msaidizi kutoka Doctors with Africa (CUAMM) Mkoa wa Simiyu, Flora Manyanda ambaye ni miongoni mwa wadau wakubwa wa shughuli mbalimbali za kijamii, ameahidi kwamba wataendelea kushirikiana na serikali ya mkoa ili kufikia mafanikio na matokea chanya.

 

Kwa upande wake, Afisa Maliasili wa Wilaya ya Itilima, Goodluck Malisa amewataka waganga wa tiba asili na mbadala kufuta taratibu za umiliki wa nyara za serikali na kuonya kuwa kumiliki au kubeba nyara za serikali bila kuwa na kibali maalumu kutoka idara ya wanyamapori Tanzania ni kinyume cha Kifungu cha 86 (1),2(b) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 kikisomwa pamoja na aya ya 14 ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

 

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Itilima)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages