NEWS

Friday 23 October 2020

DC Tarime akabidhi mamilioni kwa wanawake, vijana na walemavu

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa pili kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 62 kwa mwakilishi wa wanavikundi ikiwa ni mkopo uliotolewa leo na Halmashauri ya Mji wa Tarime kuelekezwa kwa vikundi 11 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Hamashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa.


 

HALMASHAURI ya Mji wa Tarime leo Oktoba 23, 2020 imevipatia vikundi vya wanawake, vijana na walemavu mkopo wa Sh milioni 62 kwa ajili ya kuvikwamua kiuchumi.

 

Vikundi vilivyopata mkopo huo ni 11 vikiwemo saba vya wanawake, viwili vya vijana na viwili vingine vya watu wenye ulemavu vilivyopo katika halmashauri hiyo.

 

“Siku ya leo ni muhimu sana kwetu (Halmashauri ya Mji wa Tarime) kwa sababu tunatoa mikopo ya shilingi milioni 62 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye uleavu,” amesema Mkurugenzi wa Halmashauri, Elias Ntiruhungwa na kufafanua kuwa mikopo hiyo imetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri akiwasisitiza wananchama wa vikundi vilivopata mkopo huo kuutumia fursa hiyo vizuri.

 

Akikabidhi mfano wa hundi ya mkopo huo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri amempongeza Mkurugenzi Ntiruhungwa kwa kuendelea kutoa mikopo hiyo kwa ajili ya kuwezesha kiuchumi makundi hayo ya jamii.

 

“Huu ni mfano mzuri wa jinsi serikali yenu inavyowajali,” Mhandisi Msafiri amewambia wanavikundi hao.

 

Aidha, ameipongeza halmashauri hiyo pia kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi hivyo kabla ya kutoa mikopo hiyo na kuwahimiza wanavikundi kutumia fursa ya mikopo hiyo vizuri ili kubadilisha maisha yao.

 

“Mnakopeshwa kuwezeshwa lakini mrudishe ili mkope nyingi  zaidi na wengine wakope,” Msafiri amewaambia wanavikundi hao.

 

Baadhi ya wanavikundi waliopata mkopo huo.

Wanachama wa vikundi hivyo wameishukuru serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo na kuahidi kuitumia vizuri ili kujiinua kiuchumi.

 

Sh milioni 62 zilizotolewa leo zinafanya kiasi cha mikopo iliyotolewa na Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kwa mwaka 2019/2020 kufikia Sh milioni 144, kwa mujibu wa Mkurugenzi Ntiruhungwa.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages