NEWS

Friday 9 October 2020

Kero ya maji kubaki historia mkoani Simiyu

 

 

 

 

 

 


Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maji ikiambatana na timu kutoka RUWASA zikishuhudia namna mradi wa maji ulivyowanufaisha wakazi wa kijiji Sangaitinje wilayani Meatu, Simiyu Oktoba 8, 2020.

VIJIJI 162 mkoani Simiyu vipo mbioni kuanza kunufaika na huduma ya maji baada ya kukamilika kwa miradi 71 inayotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inayotarajiwa kukamilika Desemba 2020.

Hayo yameelezwa Oktoba 8, 2020 na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala mbele ya timu ya watalaamu wa maji kutoka Wizara ya Maji katika ziara ya kukagua na tathmini miradi ya maji mkoani humo.



Mhandisi Majala amesema kukamilika kwa miradi hiyo Kutaongeza upatikanaji wa maji mkoani Simiyu ambapo tayari miradi 35 imekamilika na 36 inaendelea kutekelezwa.

"Bariadi kuna jumla ya miradi 15, kati ya hiyo, iliyokamilika ni 6 na inayoendelea kutekelezwa ni 9, Busega ipo minane - mitatu imekamilika na mitano inaendelea, Maswa ipo 14 ambapo saba imekamilika na mingine saba inaendelea kutekelezwa.

  

“Katika wilaya ya Meatu kuna miradi 11, kati ya hiyo, saba imekamilika na minne inaendelea kutekelezwa na kwa upande wa Itilima kuna miradi 23 ikiwamo 12 iliyokamilika na 11 inayoendelea kutekelezwa.


"Kati ya vijiji 162 vinavyolengwa, 75 vimeshaanza kunufaka na miradi hiyo na 87 vinatarajiwa kuanza kunufaika kuania Desemba 2020" amesema Majala.

Amefafanua kuwa miradi hiyo imeshanufaisha wananchi 200,330 na wengine 328,795 wanatarajiwa kunufaika hivi karibuni na kwamba tayari Sh bilioni 16.945 kati ya bilioni 35.317 zilitengwa zimeshatumika kwenye miradi iliyokamilika.



Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu Wizara ya Maji, Ahadi Msangi amesema kazi iliyofanywa ni kubwa na serikali imepania kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama kwa mwaka mzima.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Rasilimali za Maji amesema teknolojia ya ujenzi wa mabwawa kwenye mito ni suluhisho kwenye maeneo yenye ukame na kuongeza kuwa ujio wa mradi mkubwa wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria utasababisha tatizo la uhaba wa maji mkoani Simiyu kubaki historia.



Kwa upande wao, wanufaika wa miradi hiyo ya maji wamesema awali kabla ya kukamikika kwa miradi hiyo walitumia muda mwingi na gharama kubwa kupata huduma hiyo.

"Tulikuwa tukiamka usiku wa manane kutafuta maji, wakati mwingine tunayagombea lakini sasa hivi ni raha sana, asante Serikali ya Awamu ya Tano, Magufuli juu, juu zaidi,” amesema Jasmini Jibaka.

"Sasa hivi watu hususan wanawake wanaoga kutwa mara tatu, maji yanapatikana saa 24 kwa siku saba za wiki na tunayapata kwa bei nafuu, ndoo ya lita 20 tunauziwa kwa shilingi 50, kiukweli ni bei nafuu kabisa," amesema Mbeshy Machungwa.




(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Simiyu)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages