NEWS

Sunday 25 October 2020

Meneja Kampeni CCM: Kembaki anang’ara Tarime Mjini

Meneja Kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Joyce Mang'o akizungumza na Mara Online News leo.

 

MENEJA Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Tarime Mjini, Joyce Mang’o, amesema nyota ya mgombea ubunge wao, Michael Kembaki imezidi kung’ara na kukubalika kwa wananchi wengi jimboni humo kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

 

“Wananchi wengi wa jimbo la Tarime Mjini wameendelea kumwamini na kumkubali Kembaki, na hiyo imetokana mambo mengi ya kimaendeleo aliyotekeleza jimboni hapa kabla hajawa mbunge,” amesema Mang’o katika mahojiano maalumu na Mara Online News leo Oktoba 25, 2020.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki akijinadi kwa wananchi katika mkutano wake wa kampeni katani Nyamisangura jana.

 

Mang’o ameongeza kuwa ushirikiano thabiti wa viongozi wa CCM katika kampeni umesaidia kushawishi wana-Tarime kumwamini na kumkubali Kembaki kwamba ni kijana mpenda maendeleo anayestahili kupewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 

“Unajua wananchi wa Tarime wanapenda kiongozi wa vitendo, hawataki mtu wa blaablaa na porojo [maneno mengi bila vitendo], ndio maana tumewambia wameelewa, wamekubali na wao wenyewe wamejionea vitu vingi vya kimaendeleo ambavyo Kembaki amevifanya kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika kata zote za jimbo la Tarime Mjini,” amesisitiza.

Mamia ya wananchi wakimsikiliza na kumshangilia mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki (hayupo pichani) katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katani Nyamisangura jana.

 

Kwa mujibu wa Mang’o, hadi leo Jumapili tathmini yao [CCM] inaonesha kuwa mgombea wao, Kembaki, anakubalika kwa wananchi wengi, hali inayoashiria atashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Jumatano ijayo.

 

Joyce Mang'o akizungumzia tathmini ya kampeni za CCM jimbo la Tarime Mjini ambapo amesema inaonesha mgombea ubunge wao, Michael Kembaki anakubalika kwa wananchi wengi jimboni humo.

“Katika kampeni zetu tumefanya kazi kubwa ya kukutana na wananchi wa rika zote, na tumeweza kufanikiwa kwa asilimia kubwa, Kembaki sasa hivi anaungwa mkono na wananchi wengi hapa jimboni, tathmini yetu inaonesha ushindi wake unazidi kupaa,” amesema kampeni meneja huyo wa CCM Jimbo la Tarime Mjini.

 

(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages